The chat will start when you send the first message.
1Haleluya! Mshangilieni Bwana kule mbinguni! Mshangilieni huko juu!
2Ninyi malaika zake wote, mshangilieni! Ninyi vikosi vyake vyote, mshangilieni[#Sh. 103:20-22.]
3Jua na mwezi, mshangilieni! Ninyi nyota zote zenye mwanga, mshangilieni!
4Mbingu zilizoko juu ya mbingu, mshangilieni pamoja na maji yaliyoko mbinguni juu!
5Jina la Bwana lishangilieni! Yeye alipoagiza, ziliumbwa.[#Sh. 33:9.]
6Akazisimamisha za kuwapo kale na kale, akazikatia pao pa kuwapo, zisipapite.
7Mshangilieni Bwana huku nchini, ninyi nyama wakubwa wa baharini na vilindi vyote!
8Moto na mvua ya mawe theluji na kungugu, upepo wa kimbunga ulitimizao Neno lake,
9milima na vilima vyote, ijapo viwe vidogo, miti izaayo matunda na miangati yote,
10nyama wote wa nyumbani nao wa porini, wadudu pamoja na ndege, wao warukao,
11wafalme wa nchi na makabila yote ya watu, wakuu wao wote walio waamuzi wa nchi,
12vijana wa kiume nao wa kike, wazee pamoja nao walio watoto,
13wote pia na walishangilie Jina la Bwana! Kwani limetukuka peke yake, utukufu wake unaupita wa nchi na wa mbingu.
14Alipoyaelekeza juu mabaragumu yao walio ukoo wake, ndipo, wote waliomcha walipoyashangilia, wao wana wa Isiraeli walio ukoo wake umkaliao karibu. Haleluya![#Sh. 132:17.]