Mashangilio 15

Mashangilio 15

Mgeni wake Bwana ni nani?

(Taz. Sh. 24:3-5.)

1Bwana, yuko nani atakayetua hemani mwako? Yuko nani atakayekaa mlimani kwenye utukufu wako?[#Sh. 84:5.]

2Ni yeye ayendeleaye yaliyo sawa na kufanya yaongokayo, ni yeye awazaye moyoni mwake yaliyo kweli.[#Yes. 33:15.]

3Ulimi wake hausemi yaliyo masingizio; hamfanyizii mwenziwe kibaya, naye, waliyetua pamoja, hamtii soni.

4Aliyetupwa si kitu machoni pake, lakini wamchao Bwana anawaheshimu; kama ameapa, hageuzi, ijapo yampatie mabaya.

5Mali zake hazikopeshi, zimpatie faida nyingi, wala hatwai mapenyezo ya kumpatiliza asiyekosa. Aendeleaye hivyo hatatikisika kale na kale.[#2 Mose 22:25.]

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania