Mashangilio 28

Mashangilio 28

Kuomba wokovu pamoja na kuutukuza.

1Wewe Bwana ninakuita, u mwamba wangu, usininyamazie na kuwa kimya, nisije kufanana nao washukao kuzimuni![#Sh. 143:7.]

2Zisikie sauti za malalamiko yangu, ninapokulilia nikikuinulia mikono yangu pale Patakatifu Penyewe palipo pako![#1 Fal. 8:30; Omb. 3:41.]

3Usinipokonye pamoja nao wasiokucha, wala pamoja nao wafanyao maovu! Wao husema polepole na wenzao, lakini mioyoni mwao yamo mabaya.[#Sh. 26:9.]

4Uwape yazipasayo kazi zao na ubaya wa matendo yao, mishahara yao ipatane nayo, mikono yao yatendayo! Ndivyo, utakavyowarudishia yaliyofanyizwa nao!

5Kwani kazi zake Bwana hawazitambui, wala mikono yake iyatendayo! yawayo yote, kwa hiyo atawavunja, asiwajenge tena.[#Yes. 5:12.]

6Apasaye kutukuzwa ni Bwana, kwani huzisikia sauti zao malalamiko yangu.

7Bwana ni nguvu yangu na ngao yangu; moyo wangu ulipomwegemea, nikapata kusaidiwa. Moyo wangu ukamshangilia, nikamwimbia nyimbo za kumshukuru.[#Sh. 18:2-3.]

8Bwana ni nguvu yao, walio wake, tena ni ngome imwokoayo aliyempaka mafuta.

9Waokoe walio ukoo wako na kuwabariki watakaopata fungu kwako! Wachunge na kuwavumilia kale na kale![#Sh. 29:11.]

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania