The chat will start when you send the first message.
1Pigeni vigelegele, ninyi waongofu, kwa kuwa naye Bwana! Kumtukuza na kumsifu kunawapasa wanyokao mioyo.[#Sh. 32:11.]
2Mshukuruni Bwana na kupiga mazeze! Mpigieni nayo mapango yenye nyuzi kumi![#Sh. 92:4.]
3Mwimbieni wimbo mpya na kupiga shangwe zilizo nzuri mkizipatanisha nayo marimba![#Sh. 40:4; 96:1; 98:1; Ef. 5:19; Ufu. 5:9.]
4Kwani Bwana ayasemayo hunyoka, nayo yote ayafanyayo hutimia kweli.
5Hupenda mashauri yaongokayo, nchi imejaa magawio yake Bwana.
6Kwa neno lake Bwana mbingu zilifanyika, nayo majeshi yao yote yakatokea, alipopuzia na kinywa chake.[#1 Mose 1:6,14.]
7Maji ya bahari huyakusanya, kama yamo chunguni, navyo vilindi huviweka mahali pao.[#Sh. 104:9.]
8Sharti zimwogope Bwana nchi zote, nao wote wakaao ulimwenguni sharti wamche.
9Kwani Yeye ayasemayo mara huwapo; Yeye ayaagizayo hutokea papo hapo.
10Bwana huyavunja mashauri yao wamizimu, huyatengua mawazo yao makabila ya watu.
11Shauri lake Bwana husimama kale na kale, mawazo ya moyo wake hutimilia vizazi kwa vizazi.
12Wenye shangwe ndio, Bwana aliowawia Mungu, nalo kabila la watu, aliowachagua, wawe fungu lake.[#5 Mose 33:29.]
13Bwana huchungulia toka mbinguni, huwatazama wote pia walio wana wa watu.
14Kwenye kao lake, alikotua, huwaangalia wote wakaao nchini.
15Yeye ndiye aliyeiumba mioyo yao wote, naye ndiwe anayeyapambanua matendo yao yote.
16Hakuna mfalme aokolewaye na nguvu zake nyingi, wala fundi wa vita aponaye kwa uwezo wake mwingi.[#1 Sam. 17.]
17Farasi nao ni wa bure, hawashindi, nguvu zao nyingi haziponyi mtu.[#Sh. 20:8.]
18Utaliona jicho la Bwana, likiwatazama wamwogopao, ndio waingojeao huruma yake,[#Sh. 34:16,18.]
19aziokoe roho zao katika kufa, hata siku za njaa awatunze.[#Sh. 34:10-11.]
20Roho zetu zinamngoja yeye Bwana, ndiye msaada wetu na ngao yetu.[#Sh. 3:4.]
21Kwa hiyo mioyo yetu inamfurahia, kwani Jina lake takatifu tunaliegemea.
22Wema wako, Bwana, utukalie! Hivyo ndivyo, tunavyovingojea toka kwako.