Mashangilio 38

Mashangilio 38

Maombo ya kujutia siku za magonjwa na za maumivu ya moyo.

(Wimbo wa juto wa 3.)(Taz. Sh. 6.)

1Bwana, usinipatilize kwa ukali wako, wala kwa machafuko yako yenye moto usinichapue!

2Kwani mishale yako imenichoma, nao mkono wako umenilemea.[#Iy. 6:4; Sh. 32:4.]

3Hakuna kilicho kizima mwilini mwangu kwa ukali wako ulionitokea. Wala fupa lisilopatwa na ugonjwa haliko kabisa kwa ajili yao hayo, niliyoyakosa.[#Sh. 51:10.]

4Manza, nilizozikora, zinanirudia, nizitwike kichwani, lakini kwa kuwa mzigo upitao nguvu zangu zinanilemea.[#Omb. 1:14.]

5Madonda yangu yananuka kwa usaha mwingi kwa hivyo, nilivyokuwa mwenye upumbavu.

6Kwa kupindika sanasana nimepotoka, mchana kutwa ninatembea kwa kusikitika.

7Kwani viuno vyangu vinazidi kuchomwa na moto wa machungu, hakuna kilicho kizima mwilini mwangu.

8Nimegeuka kuwa mwembamba kwa kupondeka sanasana, moyo ukizidi kunipiga mno, ninalia.

9Bwana, unayajua yote, niyatakayo, hata ninavyopiga kite, havikujificha kwako.

10Moyo wangu unatetemeka kwa kutokwa na nguvu, nilizokuwa nazo, nao mwanga wa macho yangu haumo tena mwangu.

11Wapenzi wangu na rafiki zangu husimama mbali kwa kuviona hivyo, ninavyopatilizwa; nao walio ndugu zangu husimama mbali.[#Sh. 31:12; Iy. 19:14-19.]

12Wanaonitakia roho yangu wananitegea, wanaotafuta, watakavyoniangamiza vibaya, wanasema mapotovu, wananong'onezana madanganyifu mchana kutwa.

13Lakini mimi niko kwao kama kiziwi, nisiyasikie, au kama bubu asiyefumbua kinywa chake; ndivyo, nilivyo kwao.[#Sh. 39:3.]

14Kweli ninafanana na mtu asiyesikia, asiyeweza kubisha na kinywa chake.

15Kwani wewe Bwana ndiwe, niliyekungojea; wewe utawajibu, Bwana Mungu wangu.

16Kwani nimesema: hawatafurahi kamwe na kunicheka; kama mguu wangu ungejikwaa, wangejivuna na kunibeza.

17Kwani kuvunjika kuko karibu kwangu mimi, maumivu yangu hayakomi hata kidogo.

18Manza, nilizozikora, ninaziungama, kwa kuyasikitikia hayo, niliyoyakosa.[#Sh. 32:5.]

19Lakini adui zangu ni wenye uzima, nguvu za miili wanazo, nao wanaonichukia bure ndio wengi.

20Mema, niliyowafanyizia, wanayalipa na kunifanyizia mabaya wananipingia, kwa sababu ninayakimbilia yaliyo mema.[#Sh. 35:12.]

21Usiniache, wewe Bwana! Mungu wangu, usinikalie mbali!

22Piga mbio, unisaidie, wewe Bwana, wokovu wangu!

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania