Mashangilio 39

Mashangilio 39

Kilio cha mtu apatwaye na majaribu.

1Nilisema: Nitaziangalia njia zangu, nisiukoseshe ulimi wangu; nacho kinywa changu nitakiangalia na kukifumba, asiyemcha Mungu akingali yuko mbele yangu.[#1 Mambo 25:1,3.]

2Nikanyamaza kimya, sikusema neno; lakini hakuna chema, nilichokiona, maumivu yakazidi kunila.[#Sh. 38:14.]

3Moto ukauchoma moyo wangu kifuani mwangu, nao huo moto ukawaka na nguvu, nilipoyawaza hayo; ndipo, nilipoufungua ulimi, na useme:

4*Bwana, nijulishe mwisho utakaonipata! Niujue nao mpaka wa siku zangu, ziliokatiwa! Tena ni mbali gani kuufikia! Ya kuwa mimi ni mpitaji tu, na niyajue![#Sh. 90:12; Iy. 14:5.]

5Tazama, siku zangu, ulizonipa, ni zenye upana kama wa kiganja tu; mbele yako nipo kama mtu asiyekuwapo. Kweli kila mtu, ijapo awe mwenye nguvu, ni mvuke tu.[#Sh. 90:5.]

6Mtu hujiendea kama kivuli, mambo ya ovyoovyo huyapigia makelele, hamjui atakayezipata mali zake, lakini huzilimbika.[#Mbiu. 2:18,21; Luk. 12:18-20.]

7Sasa ningojee nini, Bwana wangu? Ninakungojea wewe peke yako.

8Katika mapotovu yangu yote niopoe, lakini usinitoe kuwa wa kusimangwa nao wapumbavu!

9Nitanyamaza tu, nisikifumbue kinywa changu, kwani wewe ndiwe uliyeyafanya.[#2 Sam. 16:10.]

10Liondoe patilizo lako, linitoke! Kwa mapigo ya mkono wako mimi nimemalizika.

11Ukimtisha mtu na kumchapua kwa ajili ya manza, unautowesha uzuri wake, kama nondo anavyofanya. Kweli kila mtu aliopo ni mvuke tu.[#Sh. 39:6.]

12Bwana, yasikie maombo yangu! Vilio vyangu sharti vifike masikioni mwako! Nayo machozi yangu usiyanyamazie! Kwani mimi ni mgeni tu apangaye kwako, kama baba zangu wote walivyokuwa.[#Sh. 119:19; 3 Mose 25:23; 1 Petr. 2:11; Ebr. 11:13.]

13Fumba macho, yasinione, uso uning'ae, nikingali sijaenda bado, nisiwepo tena!*[#Iy. 10:20.]

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania