Mashangilio 44

Mashangilio 44

Kilio cha walipotolewa.

1Mungu, tulisikia na masikio yetu, baba zetu wakituambia: Ulitenda tendo siku zao, hata siku za kale.[#5 Mose 6:20-25.]

2Wewe kwa mkono wako uliwafukuza wamizimu, ukawaweka pao, ukaangamiza makabila ya watu, upate pa kuwaenezea.

3Kwani nchi hawakuitwaa kwa nguvu za panga zao, wala mikono yao siyo iliyowashindisha, ila mkono wako wa kuume na mwanga wa uso wako ndio uliovifanya kwa kupendezwa nao.

4Wewe, Mungu, ndiwe uliye mfalme wangu; uagize wokovu, umjie Yakobo![#Sh. 74:12.]

5Kwa nguvu zako tutawakumba watusongao, waanguke; kwa nguvu za Jina lako tutawapiga mateke watuinukiao.

6Kwani siutegemei upindi wangu, kweli sio, ninaoujetea, wala upanga wangu sio uniokoao.[#Sh. 20:8.]

7Kwani wewe ulituokoa mikononi mwao watusongao, nao watuchukiao uliwatia soni.

8Mungu tunamwimbia siku zote, Jina lako tunalishukuru kale na kale.

9Na sasa umetutupa na kututia soni, maana hukutoka pamoja navyo vikosi vyetu,

10Ukaturudisha nyuma mbele yao watusongao, nao watuchukiao wakajipatia mateka;

11ukatutoa, kama tu kondoo, tuwe chakula, ukatutawanya kwao walio wamizimu.

12Walio ukoo wako umewauza kwa mali zisizo mali, lakini kwa hayo malipo yao hakuna ulichokipata.

13Ukatutia soni kwao, tuliokaa nao, tukafyozwa na kusimangwa nao waliotuzunguka.[#Sh. 79:4; 1 Fal. 9:7.]

14Ukatuweka kuwa kama fumbo kwa wamizimu, makabila ya watu hututingishia vichwa vyao.

15Siku zote hayo mabezo yapo machoni pangu; naufunika uso wangu kwa kuona soni

16nikizisikia sauti zao wanifyozao pamoja na kunitukana, nikimwona adui anitakaye, apate kujilipiza.

17Haya yote yametupata, lakini hatukukusahau, wala hatukulivunja Agano lako,

18wala mioyo yetu haikurudi nyuma, wala miguu haikuondoka katika njia yako.

19Nako, mbwa wa mwitu wanakokaa, ukatuponda, ukatufunika na giza kama la kufa.

20Kama tungekuwa tumelisahau Jina la Mungu, au kama tungekuwa tumemwinulia mungu mgeni mikono yetu,

21Mungu asingeyaumbua mambo hayo? Kwani yeye huyajua nayo mawazo yajifichayo moyoni.[#Sh. 7:10.]

22Kumbe ni kwa ajili yako wewe, tukiuawa kila siku, tukihesabiwa kuwa kama kondoo wa kuchinjwa tu![#Rom. 8:36.]

23Amka! Sababu gani umelala usingizi, Bwana wangu? Inuka! Usinitupe kale na kale![#Sh. 35:23.]

24Sababu gani unauficha uso wako? Umeyasahau maumivu yetu yatusongayo?[#Sh. 10:1.]

25Kweli roho zetu zimeinamishwa kulala uvumbini, nayo miili yetu imegandamiana na mchanga wa chini.

26Mwenye msaada, inuka, uje kwetu! Kwa ajili ya huruma yako tukomboe!

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania