Mashangilio 46

Mashangilio 46

Boma letu ni Mungu.

1*Mungu ni boma letu la kukimbilia, ni msaada wetu, tuliouona katika masongano kuwa wa kweli.

2Kwa hiyo hatuogopi, ijapo nchi iondoke, ijapo milima ianguke baharini ndani.

3Hata bahari ikivuma sana na kukuza mawimbi yake, mpaka milima itetemeke kwa kuumuka kwao: Bwana Mwenye vikosi yuko, yuko pamoja nasi, ngome yetu yenye nguvu ni Mungu wa Yakobo.

4Uko mto wa kuufurahisha mji wa Mungu kwa vijito vyake, nayo makao matakatifu yake Alioko huko juu yamo humo.[#Sh. 48:3; 2 Fal. 19:21; Yes. 12:3.]

5Mungu mwenyewe yumo mwake, hautatetemeshwa, Mungu huusaidia, kunapokucha asubuhi.

6Wamizimu walichafuka, ufalme wao ukatikisika, napo hapo, ngurumo yake yeye iliposikilika, nchi ikayeyuka.

7Bwana Mwenye vikosi yuko, yuko pamoja nasi, ngome yetu yenye nguvu ni Mungu wa Yakobo.

8Njoni, mzitazame kazi zake yeye Bwana aletaye maangamizo katika nchi yaliyo hivyo![#2 Fal. 19:35.]

9Kisha huvikomesha vita nako huko mapeoni kwa nchi akizivunja pindi na kuikatakata mikuki, akiyaunguza magari motoni.[#Sh. 76:4.]

10Acheni, mjue, ya kuwa Mungu ndio mimi! Nitatukuka kwenye wamizimu, nitatukuka nchini.

11Bwana Mwenye vikosi yuko, yuko pamoja nasi, ngome yetu yenye nguvu ni Mungu wa Yakobo.*

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania