Mashangilio 48

Mashangilio 48

Matukuzo ya Sioni.

1Bwana ni mkuu na mtukufu sana, mjini mwa Mungu wetu umo mlima wenye Patakatifu pake.[#Sh. 46:5.]

2Ni vizuri kuvitazama, unavyoinuka huo mlima wa Sioni, nchi yote nzima huufurahia; upande wa kaskazini uko mji wa mfalme mkuu.[#Omb. 2:15; Mat. 5:35.]

3Katika majumba yake mazuri Mungu amejulikana, ya kuwa ni ngome yenye nguvu.

4Tukivitazama, ni hivyo: wafalme walikula njama, wote pamoja wakaondoka kwao kupiga vita.[#2 Fal. 19.]

5Hapo walipouona, mara wakastuka, wakaingiwa na woga, wakakimbia.

6Papo hapo utetemeko ukawashika, ni uchungu kama wa mwanamke atakaye kuzaa.

7Kwa nguvu ya upepo wa kimbunga ukazivunja nazo merikebu zao za kwenda Tarsisi.

8Kama tulivyosikia, tukaviona vivyo hivyo katika mji wa Bwana Mwenye vikosi, katika mji wake Mungu wetu: Mungu ameushikiza, ukae kale na kale.

9Mungu, tunazikumbuka huruma zako Jumbani mwako.

10Kama Jina lako, Mungu, lilivyo kuu, vivyo hivyo nayo matukuzo yako yamefika mapeoni kwa nchi, mkono wako wa kuume umejaa wongofu.[#Mal. 1:11.]

11Mlima wa Sioni huufurahia, wana wa kike wa Yuda huyapigia vigelegele maamuzi yako.

12Uzungukeni mji wa Sioni na kuuzingia wote, mpate kuihesabu minara yake!

13Liangalieni boma lake, msilisahau mioyoni mwenu! Napo penye majumba yake piteni po pote, kusudi mvisimulie kizazi kijao,

14ya kuwa huyu Mungu ni Mungu wetu kale na kale pasipo mwisho. Yeye hutuongoza, mpaka tutakapokufa.[#Yes. 25:9.]

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania