Mashangilio 62

Mashangilio 62

Umnyamazie Mungu!

1Roho yangu inamnyamazia Mungu peke yake, wokovu wangu utoke kwake yeye.[#Sh. 39:1; Yes. 30:15.]

2Yeye tu ndiye mwamba wangu na wokovu wangu, ndiye ngome yangu, sitatikisika kamwe.

3Mpaka lini ninyi nyote mwamrukia mtu mmoja, mpate kumwua? mpaka awe kama ukuta unaoyumbayumba au kama kitalu kichakaacho?

4Njama zao ni kutafuta, jinsi watakavyomwondoa katika ujumbe, kwa hiyo hupendezwa na uwongo. Vinywa vyao hubariki, lakini mioyoni wanaapiza.

5Roho yangu, umnyamazie Mungu peke yake! Kwani kwake yeye ndiko, kingojeo changu kiliko.

6Yeye tu ndiye mwamba wangu na wokovu wangu, ndiye ngome yangu, sitatikisika.[#Sh. 18:2-3.]

7Wokovu wangu na utukufu wangu uliko, ndiko kwake Mungu, ni mwamba wangu wenye nguvu, kimbilio languliko kwake Mungu.[#Sh. 61:4.]

8Mwegemeeni siku zote, ninyi wenzangu wa ukoo! Imimineni mioyo yanu mbele yake! Kimbilio letu ndiye Mungu.

9Kweli wana wa watu huwa mvuke, nao ubwana wao ni wa uwongo; wakipimwa katika mizani, hupanda juu, wote pamoja ni wepesi kuliko mvuke.

10Msiuegemee ukorofi wala unyang'anyi, usiwapofushe! Mali zikiwa nyingi, msiziweke mioyoni![#Mat. 19:22; Luk. 12:19-20; 1 Tim. 6:17.]

11Mungu alisema neno moja, nimelisikia mara mbili zote, ni lile la kwamba: Nguvu ni yake Mungu.

12Wewe Bwana u mwenye upole, utamlipa mtu, kama matendo ya mtu yalivyo, ndivyo, utakavyomlipa.[#Rom. 2:6-11.]

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania