Mashangilio 68

Mashangilio 68

Mungu huwashinda wachukivu wote.

1Mungu akiinuka, hutawanyika walio adui zake, nao wamchukiao hukimbia machoni pake![#4 Mose 10:35.]

2Kama moshi unavyopeperuka, ndivyo, wanavyopeperuka; kama nta inavyoyeyuka motoni, ndivyo, wanavyoangamia usoni pake Mungu wao wasiomcha.

3Lakini waongofu hufurahi na kushangilia kwa kuchangamka na kuona furaha mbele ya Mungu.

4Mwimbieni Mungu, nalo Jina lake lishangilieni! Mtengenezeeni njia apitaye nyikani! Bwana ni Jina lake, mpigieni vigelegele![#Yes. 40:3; 57:14.]

5Ni baba yao wafiwao na wazazi, nao wajane huwaamulia, ni Mungu akaaye pake, napo ni patakatifu.[#Sh. 10:14.]

6Ni Mungu apaye wakiwa nyumba za kukaa, hutoa wafungwa kifungoni, nao wafanikiwe, lakini kwao wabishi, watakakokaa, ndiko kukavu.

7Mungu, hapo, ulipotoka kuwatangulia wao walio ukoo wako, napo hapo, ulipokwenda kukanyaga kwenye jangwa,[#2 Mose 13:21; Amu. 5:4-5.]

8ndipo, nchi ilipotetemeka, nazo mbingu zikanyesha maji, Mungu huyu alipotokea kule Sinai, alipotokea yeye Mungu aliye Mungu wao Waisiraeli.[#2 Mose 19:16-18.]

9Mvua ifurikayo ukiinyesha, Mungu, ilikuwa kila mara, fungu lako lilipotaka kuzimia; ndivyo, wewe ulivyolishikiza.

10Walio kundi lako wakapata pa kukaa, nao wanyonge ukawashikiza, Mungu, kwa wema wako.

11Wenye kulitangaza neno, alilolitoa bwana, ni kikosi kikubwa.[#Yes. 52:7.]

12Wafalme wa vikosi watakimbia, watakimbia kweli, nao wanawake wenye nyumba watagawanya mateka.

13Hapo, mnapolala kambini, yapo yanayomerimeta, yanafanana na mabawa ya kwenzi yang'aayo kama fedha, nayo manyoya yake humetuka kama dhahabu.[#Amu. 5:16.]

14Mwenyezi alipowatawanya wafalme wale, mara kuling'aa kama theluji kulikokuwa na giza kuu.[#Amu. 5:4-5; 9:4.]

15Mlima wake Mungu ni mlima wa Basani, ule mlima wa Basani ulio wenye vilima huko kileleni.

16Ninyi milima yenye vilima kileleni juu, sababu gani mnautazama kwa kijicho mlima ule Mungu alioupenda, akae pale? Kweli Bwana atakaa pale kale na kale[#Sh. 132:13.]

17Magari yake Mungu ni maelfu na maelfu, hayahesabiki, Bwana anayo kule Sinai kwenye Patakatifu pake.[#2 Fal. 6:17; Dan. 7:10.]

18Ulipopaa juu, uliteka mateka, nako kwa watu ukayapokea waliyokupa; hata wabishi hawana budi kukaa kwake Bwana Mungu.[#Ef. 4:8-10.]

19Bwana na atukuzwe siku kwa siku! Mungu hututwika mzigo, lakini hutusaidia kuuchukua.[#1 Kor. 10:13.]

20Mungu, tuliye naye, ndiye Mungu aokoaye, mwenye njia za kutoka nako kufani ni Mungu Bwana.

21Lakini vichwa vyao wachukivu wake Mungu ataviponda, nazo tosi zao wafulizao kukora manza zitachujuka.

22Bwana alisema: Nitawatoa kule Basani, niwarudishe, nitawatoa namo vilindini mwa bahari, niwarudishe.

23Ndipo, utakapoiogesha miguu yako katika damu, nazo ndimi za mbwa wako zitapata mafungu yao kwa adui zako.

24Watu huwatazama wanaokuendea, Mungu, wakimwendea patakatifu aliye Mungu wangu hata mfalme wangu.[#Sh. 24:7; 2 Sam. 6:13-14.]

25Waimbaji wanakwenda mbele, wapiga mazeze huwafuata, katikati ni wanawali wapigao patu.[#2 Mose 15:20.]

26Mnapokusanyika mtukuzeni Mungu Bwana, ninyi mnywao maji kisimani kwao Waisiraeli![#Yes. 48:1.]

27Wako wa Benyamini aliye mdogo, tena huwatawala, wako wakuu wa Yuda walio vikosi vizima, wako wakuu wa Zebuluni, nao wa Nafutali!

28Mungu wako ameviagiza vitakavyokupa nguvu; Mungu, ufulize kuyatia nguvu uliyotufanyizia!

29Kwa ajili ya Nyumba yako iliyo ya kutambika sharti wafalme wakupelekee matunzo huko Yerusalemu.[#Sh. 72:10,15.]

30karipia nyama wakaao bwawani! ndio wakorofi wote, huwa ng'ombe wakali wanaowakanyaga ndama, kwani ni fedha tu, wanazozitamani. Nayo makabila ya watu wapendao vita yatapanye kabisa!

31Ndipo, wakuu wa Misri watakapotokea, nao watu weusi, ndio watakaoviinua mikono yao kumwelekea Mungu.[#Sh. 87:4; Yes. 19:21; Tume. 8:27.]

32Mwimbieni Mungu, ninyi wafalme wa nchi, pamoja wa watu! Mshangilieni aliye Bwana!

33Ni yeye akaliaye mbingu zilizoko kule juu, nazo ni za kale, ni yeye avumishaye sauti yake, ikinguruma na nguvu.

34Mkuzeni Mungu kuwa mwenye nguvu! Waisiraeli ndio, uliowatokea utukufu wake, nguvu zake ziko juu mawinguni.[#Sh. 29:1.]

35Mungu, unaogopesha toka Patakatifu pako, Mungu wa Isiraeli; yeye ndiye atakayeupa ukoo wake nguvu za kushupaa. Na atukuzwe yeye Mungu![#Sh. 29:11.]

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania