Mashangilio 69

Mashangilio 69

Kuomba wokovu siku za kusimangwa na kusongwa.

1Na uniokoe, wewe Mungu![#Sh. 45:1.]

2Kwani yamekuja maji ya kuipata roho yangu.

3Ninazama bwawani pabonyekapo, nisione pa kusimama, nimeingia katika vilindi vya maji, mkondo wao ukanididimiza.

4Nikachoka kwa kupiga kelele, mmeo ukakauka, nikizidi kumtazamia Mungu wangu, macho yakanizimia.

5Wanaonichukia bure ni wengi kuliko nywele za kichwani pangu, adui zangu watakao kunimaliza kwa kunionea wamepata nguvu, nashurutishwa kuyarudisha nisiyoyapokonya.[#Sh. 35:19; Yoh. 15:25.]

6Wewe Mungu unaujua upumbavu wangu, nazo manza, nilizozikora, hazikufichika kwako.

7Usiache, kwa ajili yangu mimi wapatwe na soni wakungojeao wewe, Bwana Mungu Mwenye vikosi! Kwa ajili yangu mimi wasisimangike wakutafutao wewe, Mungu wa Isiraeli!

8Kwani ni kwa ajili yako wewe, nikivumilia mabezo, ijapo soni ije kuufunika uso wangu.[#Sh. 44:23.]

9Nimekwisha kuwa mgeni kwao ndugu zangu, watoto wa mama yangu hawanijui, kama si mtu wa kwao.[#Sh. 38:12; Iy. 19:13; Mat. 10:36.]

10Kwani kwa ajili ya Nyumba yako wivu unanila, nayo masimango yao wanaokusimanga yameniguia mimi.[#Yoh. 2:17; Rom. 15:3.]

11Nikalia pamoja na kujiumiza kwa kufunga, lakini wao wananisimangia navyo hivyo.

12Nikatumia gunia kuwa vazi langu, nikawa kwao kama fumbo.

13Wanaokaa langoni hunicheka, nao walevi hupiga mazeze ya kunifyoza.[#Iy. 30:9.]

14Lakini mimi ninakulalamikia, Bwana, mpaka utakapopendezwa. Mungu, kwa upole wako mwingi uniitikie na kunionyesha welekevu wako nao wokovu wako![#Yes. 49:8.]

15Nitoe kwenye matope, nipate kusimama, niokoke mikononi mwao wanichukiao namo vilindini mwa maji!

16Mkondo wa maji usinididimize, wala bwawa lisinimeze! wala kisima kisinifungie njia ya kutoka!

17Bwana, kwa upole wako ufanyao mema na uniitikie! Kwa kunionea uchungu mwingi na unigeukie!

18Usimfiche mtumishi wako uso wako! Kwani nimesongeka, usikawe kuniitikia!

19Ifikie roho yangu karibu, uikomboe! Kwa ajili ya wachukivu wangu niokoe!

20Wewe unayajua matusi na matwezo na masimango yaliyonipata, mbele yako wewe wako wote wanisongao.

21Hivyo, ninavyotukanwa vimenivunja moyo, hata nikaugua; nikangoja, kama yuko mwenye huruma, lakini hakuna; nikangoja, kama yuko mtuliza moyo, lakini sikumwona.[#Omb. 1:2,9.]

22Kilaji, walichonipa, ni maji ya nyongo, napo, nilipopatwa na kiu, walininywesha siki.[#Mat. 27:34,48.]

23Sharti meza zao ziwawie matanzi, walipizwe mabaya yao wakinaswa nayo![#Rom. 11:9-10.]

24Macho yao sharti uyafanya kuwa giza, wasione kabisa, viuno vyao sharti uvitetemeshe siku zao zote!

25Yamwage makali yako, yawapate, nao moto wa machafuko yako sharti uwafikie!

26Sharti mahame tu yawe pao pa kukaa, asioneke atakayekaa hapo, walipotua![#Tume. 1:20.]

27Kwani uliyempiga wewe, wanamkimbiza, nayo maumivu yao, uliowaumiza, wanayasimuliana.[#Yes. 53:4.]

28Waache, wajiongezee manza kwa manza, wasije kufika hapo, wongofu wako ulipo![#Rom. 1:24.]

29Sharti wafutwe katika kitabu chao walio wenye uzima, wasiandikwe pamoja nao walio waongofu![#Luk. 10:20.]

30Lakini mimi ni mkiwa mwenye maumivu, wokovu wako, Mungu, ndio utakaonitia nguvu.

31Nitalitukuza Jina la Mungu na kuliimbia, kwa kumshukuru nitamkuza.

32Hivi vitampendeza Bwana kuliko ng'ombe, ijapo awe dume lenye pembe na kwato kubwa.[#Sh. 50:8-14.]

33Maskini wakiviona watafurahi, nayo mioyo yenu ninyi mnaomtafuta Mungu na irudishwe uzimani.[#Sh. 22:27.]

34Kwani Bwana huwasikia wasio na mali, nao walio wake wakifungwa, hawabezi.

35Mbingu na nchi na zimtukuze, nazo bahari navyo vyote vinavyotembea humo!

36Kwani Mungu atauokoa Sioni atakapoijenga miji ya Yuda, watu wakae humo na kuitunza!

37Navyo vizazi vya watumishi wake vitaitwaa, nao walipendao Jina lake watakaa humo.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania