Mashangilio 74

Mashangilio 74

Kuulilia uchakavu wa Nyumba ya Mungu.

1Kwa sababu gani, Mungu, umetutupa kale na kale, moshi wa moto wa makali yako ukipanda kwao walio kondoo wako wa kuwachunga?

2Likumbuke kundi lako, ulilojipatia kale ulipolikomboa, liwe ukoo wako na fungu lako! Ukumbuke mlima wa Sioni, kao lako liliko![#Sh. 132:13.]

3Inuka, uielekeze miguu yako kuja huku kulikobomolewa kale, maana adui wamefanya, patakatifu pawe pabaya pote.

4Wabishi wako hupiga makelele pako pa kukusanyikia, wakazitweka bendera zao, zionyeshe nguvu zao.

5Tukiwatazama, wamefanana na watu wainuao mashoka juu, wakate miti iliyoko mwituni.

6Sasa mapambo yake yaliyochorwa, yote pia wanayakatakata kwa mashoka na kwa nyundo.

7Numba yako takatifu wameichoma moto, wakalichafua Kao la Jina lako mpaka chini.[#2 Fal. 25:9.]

8Walisema mioyoni mwao kwamba: Na tuwamalize wote pamoja! Nyumba za Mungu zilizoko katika nchi hii wakaziteketeza zote.[#Sh. 83:13.]

9Vielekezo vyetu hatuvioni tena, wala hakuna mfumbuaji, Kweli hakuna kwetu ajuaye, kama vitakoma lini.

10Mungu, hao watusongao watutukane mpaka lini? Adui walisimange Jina lako kale na kale?

11Mbona mkono wako unaurudisha nyuma? Utoe mkono wako wa kuume kifuani pako, uje, uwamalize!

12Lakini Mungi ni mfalme wangu tangu zamani za kale, ndiye anayetengeneza wokovu huku nchini.

13Wewe uliitenga bahari kwa nguvu yako, ukavivunja vichwa vyao nyangumi waliomo majini.[#2 Mose 14:21; 15:8-10; Hab. 3:15.]

14Wewe huviponda vichwa vyao wale papa wakubwa, ukawapa watu wakaao barani, wawalie chakula.

15Wewe hutoa mchangani visima, hata vijito, nayo majito yaliyokuwa yenye maji siku zote huyapwelesha wewe.[#Sh. 104:10.]

16Wako ni mchana, usiku nao ni wako; wewe ndiwe uliyeweka mbalamwezi nalo jua.[#Sh. 104:19; 2 Mose 17:6; Yos. 3:15-16.]

17Mipaka yote ya nchi wewe uliikata, ukaziumba siku za kiangazi nazo za kipupwe.

18Bwana, wakumbuke adui, ya kuwa hukutweza, nao watu wajinga hulibeza Jina lako.

19Roho ya hua wako usiitoe, nyama wa porini akaipata, wala usiwasahau kale na kale wanyonge wako, wawepo wenye uzima![#Ufu. 13:1.]

20Lile Agano liko, na ulitazame! Kwani maficho yote ya nchi yamegeuka kuwa makao ya ukorofi.

21Akorofikaye usimwache, ajiendee kwa kuona soni! Wanyonge na wakiwa ndio watakaolitukuza Jina lako.

22Inuka, Mungu, ujigombee kondo, kwani ni yako! Kumbuka, jinsi unavyotwezwa na wajinga siku zote![#Sh. 14.]

23Usiyasahau makelele yao wabishi wako! Mafujo yao wakuinukiao yanaongezeka siku kwa siku.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania