Mashangilio 77

Mashangilio 77

Kuomba sana msaada.

1Kwa mwimbishaji. Wimbo wa Asafu, aliomtungia Yedutuni. Nimpaliziaye sauti yangu, ndiye Mungu; ninapomwita Mungu, hunisikiliza.[#Sh. 39:1; 62:1.]

2Siku ya kusongeka kwangu nilimtafuta Bwana; mikono yangu ikawa imenyoshwa usiku kucha pasipo kulegea, maana roho yangu ilikataa kutulizwa.

3Nikimkumbuka Mungu nampigia kite, roho yangu ikitaka kuzimia, ninayawaza yote.

4Unayashika macho yangu, yasisinzie; lakini siwezi kusema kwa kuhangaika.

5Ndipo, ninapoyawaza yale mambo ya siku za kale, ndiyo yale ya ile miaka iliyokwisha kupita.[#Sh. 143:5.]

6Usiku nayakumbuka mazeze yangu humu moyoni mwangu, roho yangu ikitafuta njia ya kuyatambua hayo:

7Bwana atanitupa kale na kale? Hataendelea tena kunipendezesha?[#Sh. 85:6.]

8Huruma yake imekwisha kale na kale? Agano, aliloliwekea vizazi na vizazi, limekoma?

9Mungu ameyasahau magawio ya kuwapa watu? Au ameukataza upole wake kwa kukasirikia?

10Nikasema: Maumivu haya yananipasa, ni miaka ya mkono wake wa kuume yule Alioko huko juu.

11Haya matendo ya Bwana nitayakumbuka, navyo vioja vyako vya kale nitavikumbuka kweli.

12Ninayaweka moyoni yote, uliyoyafanya, nipate kuziwaza vema hizo kazi zako.

13Njia yako, Mungu, ni takatifu; yuko wapi aliye mungu mkuu kama Mungu?[#2 Mose 15:11.]

14Wewe ndiwe Mungu afanyaye vioja, nguvu zako hutambulikana kwa koo za watu.

15Uliwakomboa kwa mkono wako walio ukoo wako, hawa wana wa Yakobo nao wa Yosefu.

16Yalipokuona, Mungu, maji ya bahari, yalipokuona majihayo, ndipo, yalipostuka, vilindi navyo vikatetemeka.[#Sh. 104:6-7.]

17Mawingu yakanyesha mvua yenye maji mengi, mishale yako ikapiga huko na huko, nako mbinguni kukanguruma,

18Sauti za ngurumo zako zikasikilika katika kimbunga, nchini pakamulikwa na umeme, nchi ikatetemeka na kuyumbayumba.[#Sh. 18:8,14.]

19Namo baharini ndimo, njia yako ilimo, nako kwenye maji mengi ukapita, lakini nyayo zako hazikutambulika.

20Walio ukoo wako uliwaongoza kama kundi la kondoo kwa mikono yao hawa: Mose naye Haroni.[#2 Mose 12:37; 14:22.]

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania