Mashangilio 82

Mashangilio 82

Mungu huwapatiliza waamuzi wabaya.

1Mungu anasimama katika mkutano wao miungu mwingine, atoe hukumu katikati yao hiyo miungu.[#Sh. 82:6.]

2Mpaka lini mtayapotoa maamuzi yenu mkiwa upande wao wasionicha?[#5 Mose 1:17.]

3Waamulieni wakorofikao nao wafiwao na wazazi! Wanyonge na maskini watengenezeeni mashauri kwa wongofu![#Yes. 1:17.]

4Waopoeni wakorofikao nao wakiwa mkiwatoa mikononi mwao wasionicha!

5Lakini hawavitambui, wala hawaonyeki, ila hujiendea gizani, ijapo, shikizi zote za nchi zije kutikisika.

6Mimi nilisema: Ninyi m miungu, nyote m wanawe Alioko huko juu.[#Sh. 82:1; 2 Mose 21:6; Yoh. 10:34.]

7Lakini mtakufa kweli kama wana wa watu, mtaanguka kama m wenzao walio wakuu.

8Inuka, Mungu! Ihukumu nchi! Kwani mwenye wamizimu wote ndiwe wewe.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania