Mashangilio 84

Mashangilio 84

Kuitunukia Nyumba ya Mungu.

1Kwa mwimbishaji, wa kuimba kama wimbo wa wagemaji? Wimbo wa wana wa Kora.[#1 Mambo 26:1.]

2*Hapo, unapokaa, Bwana Mwenye vikosi, ndipo pazuri peke yake.

3Roho yangu ilitaka kuzimia kwa kuzitunukia nyua za Bwana; moyo wangu na mwili wangu unamshangilia Mungu Mwenye uzima.[#Sh. 25:8; 42:3,5.]

4Kumbe ndege ameona nyumba, kinega akajipatia kiota, ndimo, atakamozaa makinda yake: ndipo, unapotambikiwa wewe, Bwana Mwenye vikosi, uliye mfalme wangu na Mungu wangu.[#Sh. 5:3.]

5Wenye shangwe ndio wakaao katika Nyumba yako, wanaokushangilia pasipo kukoma.[#Sh. 65:5.]

6Wenye shangwe ndio wajitafutiao nguvu kwako wewe, wawazao mioyoni mwao, jinsi watakavyofika kwako.

7Ijapo, wapite katika bonde lilizalo wengine, hulitumia kuwa kisima cha kuwanywesha maji, kwani mvua ya vuli hulichipuza nalo na kulipatia mbaraka.[#Sh. 119:92.]

8Huendelea na kuongeza nguvu mara kwa mara, mpaka wamtokee Mungu kule Sioni na kumwambia:

9Bwana Mungu Mwenye vikosi, sikiliza ninayokuomba! Tega masikio, Mungu wa Yakobo!

10Mungu uliye ngao yetu, unitazame, uuone uso wake uliyempaka mafuta![#Sh. 72:15.]

11Kwani siku moja ya kukaa katika nyua za Bwana ni nzuri kuliko nyingine, ijapo ziwe elfu. Kungoja zamu mlangoni kwa nyumba ya Mungu kwanipendeza kuliko kukaa mahemani kwao wasiomcha Mungu.[#Sh. 27:4.]

12Kwani Bwana Mungu ni jua na ngao, Bwana hutugawia nao utukufu, wanaoendelea wakimcha hawanyimi chema cho chote.[#Sh. 3:4; 34:11.]

13Mtu akuegemeaye, Bwana Mwenye vikosi, ndiye mwenye shangwe.*

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania