Mashangilio 9

Mashangilio 9

Kuomba msaada wa Mungu apatilizaye wachukivu wasiomcha.

1Nitamshukuru Bwana kwa moyo wangu wote, nitayasimulia mataajabu yako, uliyoyafanya yote.

2Kwa kufurahi nitakushangilia, nitaliimbia Jina lako wewe ulioko huko juu,

3kwani adui zangu wamerudi nyuma, wakajikwaa, wakaangamia machoni pako.

4Maana umenipatia kushinda, nilipohukumiwa, ukakalia kiti cha uamuzi, utoe hukumu iongokayo.[#Sh. 7:12.]

5Umekaripia wamizimu, ukaangamiza wasiokucha, ukayafuta majina yao, yasiwepo tena kale na kale.

6Adui wamemalizika, nako walikokaa kutakuwa na maheme tu kale na kale, maana miji yao umeibomoa, kumbuko lao likaangamia.[#Sh. 34:17.]

7Bwana hukaa kale na kale, akakisimika kiti chake, atoe hukumu.[#Sh. 103:19.]

8Yeye ndiye atakayeuhukumu ulimwengu kwa wongofu, ayaamue makabila ya watu kwa unyofu.[#Sh. 96:13.]

9Hivyo Bwana ni ngome yao waliokorofika, katika siku za masongano ni ngome kweli.

10Walijuao Jina lako watakuegemea, kwani wanaokutafuta, Bwana, huwaachi.

11Mshangilieni Bwana akaaye Sioni! Tangazeni matendo yake kwenye makabila ya watu![#Sh. 132:13.]

12Kwa kuwa ni mwenye kulipiza damu, huwakumbuka, malalamiko yao wakiwa hayasahau.[#1 Mose 4:10.]

13Nihurumie, Bwana, ukitazama, ninavyoteswa nao wanaonichukia! Maana aliyenikweza na kunitoa malangoni mwa kufa ni wewe.

14Hivyo nitayasimulia matukuzo yako yote malangoni mwa binti Sioni na kupiga vigelegele, kwa sababu umeniokoa.[#Sh. 13:5; 22:23; 40:10-11.]

15Wamizimu wamedidimia katika shimo, walilolifanya wao, miguu yao ikanaswa katika tanzi, walilolitega wenyewe.[#Sh. 7:16.]

16Hivyo Bwana hujulika anapofanya hukumu, huwanasa kwa kazi za mikono yao wao wasiomcha.[#Sh. 7:17.]

(Hapa yapigwe mazeze tu. Kituo)

17Wasiomcha Mungu watarudi kuzimuni, nao wamizimu wote pamoja nao wanaomsahau Mungu.

18Kwani mkiwa hasahauliwi kale na kale, wala kingojeo chao wanyonge hakiangamii zamani zote.[#Sh. 10:17-18; 22:25.]

19Inuka, Bwana, watu wasikaze nguvu, wamizimu wahukumiwe machoni pako!

20Wakemee wamizimu, Bwana, kusudi wastushwe, kusudi wajitambue kuwa watu tu![#Sh. 59:14.]

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania