Mashangilio 90

Mashangilio 90

Kitabu cha nne.

Mungu ni kimbilio letu.

1Bwana, wewe ndiwe kimbilio letu kwa vizazi na vizazi.

2Milima ilipokuwa haijazaliwa bado, hata nchi na ulimwengu zilipokuwa hazijaumbwa bado, wewe Mungu ulikuwa uko tangu kale hata kale.

3Unawageuza watu kuwa mavumbi tena ukiwaambia: Rudini, ninyi wana wa watu![#1 Mose 3:19; Mbiu. 1:4; 12:7.]

4Kwani machoni pako miaka elfu ni kama siku ya jana, ikiisha kupita, au kama zamu moja ya usiku.[#2 Petr. 3:8.]

5Kama watu wanavyochukuliwa na maji, ndivyo, unavyowadidimiza; kama usingizi wa asubuhi ulivyo, ndivyo, walivyo nao, au kama maua yanayochanua upesi:[#Sh. 102:12; 103:15; Iy. 14:2; Yes. 40:6-7.]

6asubuhi hupasua na kuchanua, jioni hupakatika na kunyauka.

7Kwani tunamalizika kwa makali yako, maana tunatoweshwa na moto wa machafuko yako.

8Manza, tulizozikora, unaziweka machoni pako, makosa, tuliyoyaficha, hutokea mwangani mwa uso wako.

9Kwa hiyo siku zetu zote zinapita upesi kwa machafuko yako, tunaimaliza miaka yetu kuwa kama mapuzi tu.

10Siku zetu za kuwapo ni miaka sabini, kama tunazidi kuwa wenye nguvu, ni miaka themanini. Nayo masumbuko na mateso ndio urembo wao; kwa kuwa tunaruka kama ndege, zinapita upesi.[#Mbiu. 1:3,8.]

11Lakini yuko nani azitambuaye nguvu za makali yako? Tena yuko nani ayaogopaye hayo machafuko yako?

12Tufundishe kuzihesabu siku zetu, tujipatie mioyo yenye ujuzi![#Sh. 39:5; 1 Mose 47:9; Rom. 6:23.]

13Rudi, Bwana! Utatukalia mbali mpaka lini? Walio watumishi wako wahurumie!

14Tushibishe upole wako kila kunapokucha! Ndivyo, tutakavyoshangilia kwa furaha siku zetu zote.

15Siku za kutufurahisha ziwe sawasawa nazo, ulizotutesa, ziwe miaka mingi, kama ilivyokuwa ile ya kuona mabaya.

16Matendo yako na yaonekane kwa watumishi wako, nao utukufu wako kwa wana wao!

17Nao wema wake Bwana Mungu wetu na utukalie! Kazi za mikono yetu zifanikishe kwetu! Kazi za mikono yetu uzifanikishe kweli!*

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania