The chat will start when you send the first message.
1Akaaye fichoni kwake alioko huko juu, alalaye kivulini kwake aliye Mwenyezi
2humwambia Bwana: Kimbilio langu, tena ngome yangu, Mungu wangu, nimwegemeaye![#Sh. 18:3.]
3Kwani yeye ndiye aniokoaye tanzini mwa mwindaji, namo mwenye kipindupindu kiangamizacho.[#Sh. 124:7.]
4Kwa manyoya yake atakufunika, namo mabawani mwake ndani utakimbilia, welekevu wake ni ngao, hata kingio.
5Hutaogopa mastusho ya usiku, wala mshale upigwao mchana,
6wala kipindupindu kinyatiacho gizani, wala magonjwa mengine mabaya yauayo na mchana.
7Kama wataanguka elfu zima upande wako, au maelfu kumi kuumeni kwako, lakini kwako wewe hayatafika.
8Kweli, macho yako yenyewe yatavitazama; jinsi wasiomcha Mungu wanavyolipishwa, utaviona.[#Sh. 54:9.]
9Kwani wewe ulisema: Bwana ni kimbilio langu, naye Alioko huko juu unamtumia kuwa kao lako.
10Hakuna kibaya kitakachokufikia mwako nyumbani, wala hakuna pigo litakalokikaribia kituo chako.
11Kwani atakuagizia malaika zake, wakulinde katika njia zako ziwazo zote.[#Mat. 4:6.]
12Nao watakuchukua mikononi mwao, usije kujikwaa mguu wako katika jiwe.
13Utakanyaga simba nao nyoka, utaponda kwa mateke wana wa simba nao nondo.[#Luk. 10:19.]
14Kwa kuwa ameshikamana na mimi, nitamwopoa, kwa kuwa analijua Jina langu, nitamkweza.
15Atakaponiita, nitamwitikia, mimi niko pamoja naye katika masongano, nimwokoe, kisha nimpe hata utukufu.
16Wingi wa siku zake za kuwapo ndio, nitakaomshibisha, nimchangamshe, akiuona huo wokovu wangu.