Mashangilio 92

Mashangilio 92

Kuushukuru wongofu wake Mungu.

1Ni kitu kizuri kumshukuru Bwana na kuliimbia Jina lako, ulioko huko juu,[#Sh. 147:1.]

2asubuhi kuutangaza upole wako, tena usiku welekevu wako

3kwa kupiga mapango yenye nyuzi kumi pamoja na mazeze yaliayo vizuri.[#Sh. 33:2.]

4Kwani, wewe Bwana, umenifurahisha kwa matendo yako, kazi za mikono yako ninazishangilia.

5Kazi zako, Bwana, ni kubwa peke yao, mawazo yako ni marefu mno, hayachunguziki.[#Sh. 104:24; Yes. 55:9.]

6Lakini mtu asiyejua kitu hayatambui, wala mpumbavu hayaoni hayo.

7Wasiomcha Mungu wakichipuka kama majani, nao wote wafanyao maovu wakichanua vizuri, ni kwamba tu: Sharti waangamizwe kale na kale.[#Sh. 37:2.]

8Wewe, Bwana, unatukuka kale na kale.[#Sh. 97:9.]

9Kwani, Bwana, ukiwatazama wao wachukivu wako, ukiwatazama vema wao wachukivu wako, mara hupotea, wote wafanyao maovu hutawanyika.

10Lakini baragumu langu umelielekeza juu kama pembe za nyati, nikafurikiwa na mafuta ya mwaka huu.[#Sh. 23:5.]

11Macho yangu yataona furaha kwao walioninyatia, masikio yangu yatayasikia na kiyafurahia, wabaya walioniinukia waliyofanyiziwa.[#Sh. 91:8.]

12Mwongofu atachipuka kama mtende, atakua kama mwangati ulioko Libanoni.[#Sh. 52:10.]

13Kwenye Nyumba ya Bwana wako wlaiopandwa huko, watachipuza matawi katika nyua zake Mungu wetu;[#Sh. 84:3.]

14ijapo, wawe wazee, wataendelea kuzaa, maana watakuwa wenye utomvu na majani mengi.[#Sh. 1:3.]

15Hivyo watautangaza unyofu, Bwana alio nao; mwake yeye aliye mwamba wangu hamna upotovu.[#5 Mose 32:4.]

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania