Mashangilio 96

Mashangilio 96

Kumshukuru Mungu aliye mwenye kuzihukumu nchi zote.

(Taz. 1 Mambo 16:23-33.)

1*Mwimbieni Bwana wimbo mpya! Mwimbieni Bwana, nchi zote![#Sh. 33:3.]

2Mwimbieni Bwana! Likuzeni Jina lake! Utangazeni wokovu wake siku kwa siku!

3Wasimulieni wamizimu utukufu wake nako kwenye makabila yote ya watu mataajabu yake!

4Kwani mkuu ni Bwana, apaswa na kutukuzwa sana, naye anaogopesha kuliko miungu yote.

5Kwani miungu yote ya makabila ya watu ni ya bure tu, lakini Bwana ndiye aliyezifanya mbingu.

6Ukuu na urembo uko mbele yake, uwezo na utukufu upo Patakatifu pake.

7Ninyi mlio wa ukoo wa watu, mpeni Bwana yaliyo yake! Kwa kuwa ni mtukufu na mnguvu, mpeni Bwana yaliyo yake!

8Kwa kuwa jina lake ni tukufu, mpeni Bwana yaliyo yake! Chukueni vipaji vya tambiko, mje kuziingia nyua zake![#Sh. 72:10.]

9Mtambikieni Bwana na kuvaa mapambo yapasayo Patakatifu! Mkimtokea, mastuko na yawaguie, ninyi wa nchi zote!

10Tangazeni kwa wamizimu kwamba: Bwana ni mfalme! Yeye ndiye aliyeishikiza nchi, isije kuyumbayumba, yeye ndiye atakayewaamulia watu maamuzi yanyokayo.*[#Sh. 93:1.]

11Kwa hiyo mbingu na zifurahi, nchi nayo na ipige shangwe! Hata bahari nayo yote yajaayo ndani yake na yavume![#Sh. 98:7-9; Yes. 49:13.]

12Mashamba nayo yote yaliyomo na yapige vigelegele! Itakuwa, nayo miti yote ya mwituni imshangilie Bwana,

13kwani ndiye atakayekuja kweli kuihukumu nchi, atauhukumu ulimwengu kwa wongofu, nayo makabila ya watu kwa welekevu wake.[#Tume. 17:31.]

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania