Ufunuo 16

Ufunuo 16

Mapigo matatu ya kwanza.

1Nikasikia sauti kuu iliyotoka Jumbani mwa Mungu, ikiwaambia wale malaika saba: Nendeni, mvimwage nchini vile vyano saba vya makali ya Mungu![#Ufu. 15:7.]

2Pakaondoka wa kwanza, akakimwaga chano chake nchini. Ndipo, majipu maovu na mabaya yalipowatokea hao waliokuwa na chapa cha yule nyama, nao waliokiangukia kinyago chake.[#2 Mose 9:10-11.]

3Wa pili alipokimwaga chano chake baharini, ndipo, ilipogeuka kuwa damu kama ya mfu; kwa hiyo vikafa mle baharini vyote vilivyokuwamo vyenye uzima.[#2 Mose 7:17-21.]

4Wa tatu alipokimwaga chano chake katika mito na katika chemchemi za maji, ndipo, nayo yalipogeuka kuwa damu.[#2 Mose 7:19-24.]

5Kisha nikamsikia yule malaika wa maji, akisema: Wewe u mwongofu, uliopo, uliyekuwapo, unatakata, kwa kuwa umehukumu hivyo:

6waliomwaga damu za watakatifu na za wafumbuaji umewapa damu, wazinywe; ndivyo, ilivyowapasa.

7Kisha nikaisikia meza ya Bwana, ikisema: Kweli Bwana Mungu Mwenyezi, hukumu zako ni za kweli na za wongofu.[#Ufu. 9:13; 19:2.]

Pigo la nne na la tano.

8Wa nne alipokimwaga chano chake juani, ndipo, lilipopewa kuwaunguza watu kwa moto.

9Lakini watu walipounguzwa kwa kuchomwa na moto sana wakalitukana Jina la Mungu aliyekuwa na nguvu ya mapigo hayo, wakakataa kujuta na kumtukuza yeye.[#Ufu. 9:20-21; 16:11,21.]

10Wa tano alipokimwaga chano chake kitini mwa kifalme mwa yule nyama, ndipo, ufalme wake ulipotiwa giza, wenyewe wakaziuma ndimi zao kwa kuumia sana,[#2 Mose 10:21; Yes. 8:21-22.]

11wakamtukana Mungu wa mbingu kwa ajili ya maumivu yao, na ya majipu yao, wakakataa kujuta na kuyaacha matendo yao.[#Ufu. 16:9.]

Pigo la sita na la saba.

12Wa sita alipokimwaga chano chake mle katika mto mkubwa wa Eufurati, ndipo, maji yake yalipokupwa, kusudi njia itengenezwe ya wafalme watakaotoka maawioni kwa jua.[#Ufu. 9:14; Yes. 11:15-16.]

13Nikaona pepo tatu zenye uchafu, zikitoka domoni mwa yule joka namo domoni mwa yule nyama namo domoni mwa yule mfumbuaji wa uwongo, zikawa kama vyura;[#Ufu. 12:3,9; 13:1,11-14; 2 Mose 8:3,7,11; 1 Fal. 22:21-23.]

14kwani ndizo roho za pepo zinazofanya vielekezo. Zikawatokea wafalme wa ulimwengu wote, ziwakusanye kupiga vita, siku kubwa ya Mungu Mwenyezi itakapotimia.[#Ufu. 13:13; 19:19.]

15Tazama, ninakuja kama mwizi. Mwenye shangwe ndiye atakayekesha na kuziangalia nguo zake, asitembee mwenye uchi, watu wakiyaona yake yenye soni.[#Ufu. 3:18; 1 Tes. 5:2.]

16Lakini zile pepo zikawakusanya wafalme mahali panapoitwa Kiebureo: Harmagedoni.[#Amu. 5:19,31; 2 Fal. 9:27; 23:29; Zak. 12:11.]

17Wa saba alipokimwaga chano chake angani, ndipo, sauti kuu ilipotoka Jumbani mwa Mungu upande wa kiti cha kifalme ikisema: Imekwisha kufanyika!

18Kukapiga umeme na uvumi na ngurumo, kisha kukawa tetemeko kubwa la nchi kupita yote yaliyokuwapo; tangu hapo, mtu alipokaa nchini, halikuwapo tetemeko lililokuwa kubwa kama hilo.[#Ufu. 4:5; 8:5; 11:19.]

19Ndipo, ule mji mkubwa ulipogawanyika kuwa mafungu matatu, hata miji ya wamizimu ikaanguka. Ndipo, nao mji mkubwa wa Babeli ulipokumbukwa mbele ya Mungu, upewe kinyweo cha mvinyo chungu ya makali yake.[#Ufu. 11:8; 14:8,10.]

20Navyo visiwa vyote vikatoweka, hata milima haikuonekana tena.[#Ufu. 6:14; 20:11.]

21Kisha mvua kubwa ya mawe mazito yalinganayo na makonde ikawanyeshea watu toka mbinguni. Lakini watu wakamtukana Mungu kwa ajili ya pigo kuu la mvua ya mawe, kwani pigo lake lilikuwa kubwa mno.[#Ufu. 16:9; 2 Mose 9:23.]

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania