Ufunuo 18

Ufunuo 18

Mapatilizo ya Babeli.

1Kisha nikaona malaika mwingine, akishuka toka mbinguni mwenye nguvu kuu, nchi ikaangazwa na utukufu wake.[#Ufu. 10:1; Ez. 43:2.]

2Akapaza sauti kwa nguvu akisema: Umeanguka! Umeanguka mji mkubwa wa Babeli! Umegeuka kuwa kao la mashetani na ngome ya pepo zote wenye uchafu na ya ndege wabaya wote wachukiwao.[#Ufu. 14:8; Yes. 13:21; 34:11,13; Yer. 50:39.]

3Kwani wamizimu wote wamekunywa mvinyo mkali za ugoni wake, wafalme wa nchini wakafanya ugoni naye, wachuuzi wa nchini wakapata mali nyingi kwa hivyo, alivyokaza kuyatapanya yaliyokuwa yake.[#Ufu. 14:8; Yer. 51:7; Nah. 3:4.]

4Kisha nikasikia sauti nyingine iliyotoka mbinguni kwamba: Enyi mlio watu wangu, tokeni kwake! Maana msiwe wenzake wa makosa yake, wala msipate nanyi mapigo yake![#Yes. 48:20; 52:11; Yer. 50:8; 51:6,45.]

5Kwani makosa yake hugandamiana, yamefika hata mbinguni, Mungu akayakumbuka mapotovu yake.[#1 Mose 18:20-21; Yer. 51:9.]

6Mlipeni, kama alivyolipa mwenyewe! Mlipeni mara mbili kwa hivyo, matendo yake yalivyokuwa! Kinyweo kile, alichowatia, mtieni yeye mara mbili![#Sh. 137:8; Yer. 50:15,29.]

7Kwa hivyo, alivyojitukuza na kuyatapanya yaliyo yake, kazeni vivyo hivyo kumtesa na kumwumiza! Kwa sababu husema moyoni mwake: Nafuliza kuwa mfalme wa kike, nami si mwanamke mjane, wala sitaona masikitiko kamwe.[#Yes. 47:7-8; Yer. 50:29.]

8Kwa hiyo mapigo yake yatamjia yote siku moja, kufiwa na kusikitika na kuumwa na njaa; kisha atateketezwa kwa moto kabisa. Kwani Bwana Mungu atakayemhukumu ni mwenye nguvu.[#Ufu. 17:16; Yes. 47:8-9; Yer. 50:31.]

Kilio cha kuulilia mji wa Babeli.

9Ndipo, wafalme wa nchini waliofanya naye ugoni na kuyatapanya yalio yake watakapomlilia na kumwombolezea, watakapouona moshi wa kuteketea kwake.[#Ufu. 17:2.]

10Watasimama mbali kwa ajili ya kuyaogopa maumivu yake wakisema: Mama we! Mama we! Mji huu mkubwa wa Babeli! Mji huu wenye nguvu![#Ufu. 14:8; Yes. 21:9; Yer. 51:8.]

11Kwa saa moja umekwisha kuhukumiwa! Wachuuzi wa nchini watalia nao na kuomboleza kwa ajili yake, kwani hakuna tena atakayezinunua bidhaa zao,[#Ez. 27:36.]

12zile za dhahabu na za fedha na za vito na za ushanga na za nguo na za bafta na za nguo za kifalme na za hariri na za rangi nzuri, tena ile miti yote ya kuvukiza na vyombo vyote vya pembe na vya mpingo na vya shaba na vya chuma na vya mawe meupe sana,[#Ez. 27:12-13,22.]

13tena dalasini na karafuu na manukato na uvumba na ubani na mvinyo na mafuta na unga mzuri na ngano na ng'ombe na kondoo na farasi na magari, nayo miili na roho za watu.

14Hata matunda yako, uliyoyatunukia kwa roho yako, yamekutoka wewe, navyo vyote vilivyokunonesha na kuung'aza mwili vimekupotelea, hutaviona tena.

15Wachuuzi wa vitu hivyo waliovipatia mali nyingi kwake watasimama mbali kwa ajili ya kuyaogopa maumivu yake wakilia na kuomboleza

16na kusema: Mama we! Mama we! Mji huu mkubwa uliovaa nguo za bafta na za kifalme na za rangi nzuri na kujipamba na dhahabu na vito na ushanga![#Ufu. 17:4.]

17Kwa saa moja huo uzuri uliokuwa mwingi hivyo umeangamika wote! Nao wakuu wa merikebu nao wenye vyombo vidogo na wabaharia wote nao wote wanaofanya kazi baharini walisimama mbali,[#Yes. 23:14; Ez. 27:27-29.]

18wakapiga kelele walipouona moshi wa kuteketea kwake wakisema: Uko wapi mji unaofanana na na mji huu mkubwa?[#Yes. 34:10.]

19Wakajitupia mavumbi vichwani pao, wakapiga kelele wakilia na kuomboleza na kusema: Mama we! Mama we! Mji huu mkubwa! Katika malimbiko yako ndimo, wote walio na vyombo baharini walimopata mali nyingi! Kwa saa moja umeanguka![#Ez. 27:30-34.]

20Shangilieni kwa ajili yake, enyi mbingu, nanyi watakatifu na mitume na wafumbuaji! Kwani Mungu ameulipiza mapatilizo yenu.[#Yes. 44:23; Yer. 51:48.]

Kutupwa kwake Babeli.

21Kisha malaika mmoja mwenye nguvu akainua jiwe kama jiwe kubwa la kusagia, akalibwaga baharini akisema: Kwa nguvu kama hii mji mkubwa wa Babeli utabwagwa upesi hivyo, usionekane tena.[#Yer. 51:63-64.]

22Namo mwako hamtasikilika tena sauti zao wapigao mazeze na ngoma na filimbi na mabaragumu, wala hamtaonekana tena mwako fundi aliye yote wa kazi yo yote, wala hamtasikilika tena mwako sauti ya kusaga,[#Yes. 24:8; Ez. 26:13.]

23wala hamtamulika tena mwako mwanga wa taa, wala sauti ya mchumba wa kiume na wa kike haitasikilika tena mwako. Kwani wachuuzi wako walikuwa wakuu wa nchi, kwani kwa uchawi wako wamizimu wote walipotezwa.[#Yes. 23:8; Yer. 7:34; 16:9; 25:10.]

24Damu za wafumbuaji na za watakatifu nazo zao wote waliouawa nchini zilionekana mwake.[#Ufu. 6:10; 17:6; 19:2; Mat. 23:35,37.]

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania