The chat will start when you send the first message.
1Kisha akanionyesha mto wa maji ya uzima wenye kumetuka kama kito, ulitoka penye kiti cha kifalme cha Mungu na cha Mwana kondoo.[#Ez. 47:1; Zak. 14:8.]
2Uwanjani katikati na kandokando ya mto pande zote mbili kulikuwa na miti ya uzima izaayo matunda mara kumi na mbili, kila mwezi hutoa matunda yao, nayo majani ya miti ndiyo yanayowapa wamizimu uzima.[#Ufu. 21:21; Ez. 47:12.]
3Hapatakuwapo tena chenye mwiko cho chote. Kiti cha kifalme cha Mungu na cha Mwana kondoo kitakuwamo humo mwake, nao watumwa wake watamtumikia[#Yos. 7:11-13; Zak. 14:11.]
4na kumwona uso wake, hata Jina lake litakuwa mapajini pao.[#Ufu. 3:12; 21:3.]
5Usiku hautakuwapo tena, wala hawatautumia tena mwanga wa taa wala mwanga wa jua, kwani Bwana Mungu atawamulikia; hivyo watatawala kale na kale pasipo mwisho.[#Ufu. 5:10; 21:25; Dan. 7:18,27.]
6Kisha akaniambia: Maneno haya yapasa kutegemewa, maana ni ya kweli, naye Bwana Mungu wa roho za wafumbuaji amemtuma malaika wake, awaonyeshe watumwa wake yatakayofanyika upesi.[#Ufu. 1:1; 4 Mose 27:16; 1 Kor. 14:32.]
7Tazama, ninakuja upesi! Mwenye shangwe ndiye atakayeyashika maneno ya ufumbuo wa kitabu hiki.[#Ufu. 1:3; 3:11; 22:12,20.]
8Nami Yohana nimeyasikia, tena nimeyaona mambo haya. Nami nilipoyasikia na kuyaona nikaanguka kusujudu penye miguu ya yule malaika aliyenionyesha mambo haya.[#Ufu. 19:10.]
9Akaniambia: Angalia, sivyo! Mimi ni mtumwa mwenzenu wewe na ndugu zako walio wafumbuaji nao wanaoyashika maneno ya kitabu hiki. Umwangukie Mungu!
10Kisha akaniambia: Usiyafiche maneno ya ufumbuo wa kitabu hiki na kuyafunga kwa kutia muhuri! Kwani siku ziko karibu.[#Ufu. 1:3; 10:4; Dan. 8:26; 12:4.]
11Mwenye kupotoa na afulize kupotoa! Naye mwenye uchafu na afulize kujichafua! Lakini mwenye wongofu na afulize kuyafanya yaongokayo! Naye mwenye kutakata na afulize kujitakasa![#Dan. 12:10.]
12Tazama, naja upesi, nao mshahara wangu wa kuwalipa ninyi uko pamoja nami, nimlipe kila mmoja, kama kazi yake ilivyo.[#Ufu. 3:11; 22:7; Yes. 40:10; Rom. 2:6.]
13Mimi ni A na O, wa kwanza na wa mwisho, mwanzo na mwisho.[#Ufu. 1:11; Ebr. 13:8.]
14Wenye shangwe ndio waliozifua nguo zao, wapewe kuufikia mti wa uzima na kuingia malangoni mwa ule mji.[#Ufu. 12:17.]
15Nje wako mbwa na wachawi na wagoni na wauaji na watambikia vinyago, nao wote wapendao uwongo na kuufanya.[#Ufu. 21:8,27; 1 Kor. 6:9-10; Fil. 3:2.]
16Mimi Yesu nimemtuma malaika wangu, awashuhudie haya penye wateule. Mimi ni mzizi na mzao wa Dawidi, ile nyota imulikayo mapema.[#Ufu. 1:1-2; 5:5; Yes. 11:10; Luk. 1:78.]
17Roho naye mchumba mke wanasema: Njoo! Naye mwenye kusikia na aseme: Njoo! Naye mwenye kuona kiu na aje! Naye ayatakaye na ateke bure maji ya uzima![#Ufu. 21:6; Yes. 55:1; Yoh. 7:37; Rom. 8:23.]
18Mimi namshuhudia kila ayasikiaye maneno ya ufumbuo wa kitabu hiki: Mtu atakayeyaongeza maneno haya, Mungu atamwongezea mapigo yaliyoandikwa katika kitabu hiki.[#Ufu. 15:1,6.]
19Naye atakayeyapunguza maneno ya kitabu cha ufumbuo huu, Mungu ataliondoa fungu lake penye mti wa uzima namo mwenye mji mtakatifu, kama ilivyoandikwa katika kitabu hiki.[#Ufu. 22:2; 5 Mose 4:2.]
20Anayeyashuhudia haya anasema: Kweli, ninakuja upesi, Amin. Njoo, Bwana Yesu!
21Upole wa Bwana Yesu uwakalie ninyi nyote! Amin.