Waroma 10

Waroma 10

Wayuda waliukataa wongofu wa Mungu.

1*Ndugu, moyo wangu unayapenda sana, ninayomwomba Mungu kwamba: Waisiraeli waokoke.

2Kwani nawashuhudia, ya kuwa waona wivu kwa ajili yake Mungu, lakini hawamtambui.

3Kwani wongofu, Mungu anaoutaka, hawaujui, wakajaribu kujiongoza wenyewe, lakini hivyo hawakuutii ule wongofu, Mungu anaoutaka.[#Rom. 9:31-32.]

4Kwani timilizo la Maonyo ni Kristo, kila mwenye kumtegemea ajipatie wongofu![#Mat. 5:17; Yoh. 1:17; 3:18; Gal. 3:24-25; Ebr. 8:13.]

5Kwani Mose aliandika:

Anayeufanya wongofu ulioagizwa na Maonyo

mtu huyo atapata uzima kwa njia hiyo.

6Lakini wongofu unaopatikana kwa kumtegemea Mungu unasema hivyo: Usiseme moyoni mwako: Yuko nani atakayepaa kwenda mbinguni? Huko ndiko kumshusha Kristo.[#5 Mose 30:12-13.]

7Wala usiseme: Yuko nani atakayeshuka kwenda kuzimuni? Huko ndiko kumpaza Kristo na kumtoa kwenye wafu.

8Tena unasema:

Neno hilo linakukalia karibu, limo kinywani mwako,

namo moyoni mwako.

Hilo ndilo neno la kumtegemea Mungu, ni hilihili, tunalolitangaza.

9Kwani ukiungama kwa kinywa chako kwamba: BWANA NI YESU, ukamtegemea kwa moyo wako kwamba: Mungu alimfufua katika wafu, utaokoka.[#2 Kor. 4:5.]

10Kwani ukimtegemea kwa moyo unapata wongofu; ukimwungama kwa kinywa unaokoka.

11Kwani Maandiko yasema: Kila anayemtegemea hatatwezeka.[#Yes. 28:16.]

12Kwani hapa hawachaguliwi Wayuda na Wagriki; kwani aliye Bwana wao wote ni yuyu huyu mmoja, ni mwenye magawio yanayowatoshea wote wanaomtambikia.[#Tume. 10:34; 15:9.]

13Kwani;

Kila atakayelitambikia Jina la Bwana ataokoka.

14Basi, watamtambikiaje, wasiyemtegemea? Tena watamtegemeaje, ambaye hawajamsikia Neno lake? Tena watasikiaje, pasipokuwapo mwenye kutangaza?

15Tena watatangazaje, wasipotumwa? Ndivyo ilivyoandikwa:

Tazameni, miguu yao wapiga mbiu njema jinsi inavyopendeza!*

16Lakini walioutii huo Utume mwema sio wote. Kwani Yesaya anasema:

Bwana, yuko nani anayeutegemea utume wetu?

17Basi, kumtegemea Mungu huletwa na matangazo, lakini matangazo hutoka katika Neno la Kristo.[#Yoh. 17:20.]

18Lakini niseme: Hawakusikia? Kusikia wamesikia.

Uvumi wao ulitokea katika nchi zote;

nayo maneno yao yalifika hata mapeoni kwa ulimwengu.

19Au niseme: Waisiraeli hawakulitambua? Kwanza Mose anasema:

Mimi na niwachokoze ninyi nikiwaletea watu wasio watu,

na niwakasirishe ninyi nikiwaletea taifa la watu

wasiojua maana.

20Kisha Yesaya anajipa moyo wa kusema:

Nimeonwa nao wasionitafuta, nikawatokea wasioniuliza.

21Lakini Waisiraeli anawaambia:

Mchana kutwa naliikunjua mikono yangu,

nipungie ukoo wa watu wasioonyeka, walio wabishi tu.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania