Wimbo mkuu 1

Wimbo mkuu 1

Mpenzi mke na mume wanaopendana.

1Na aninonee kwa manoneo ya kinywa chake!

2Kwani upendo wako hupendeza kuliko mvinyo.

3Mafuta yako ya kupaka hunukia vema,

jina lako ni mafuta yaliyomiminwa,

kwa hiyo wanawali hukupenda.

4Nivute, nikufuate nyuma! Na tupige mbio!

Hata mfalme akiniingiza vijumbani mwake,

na tupige vigelegele kwa kukufurahia wewe!

Huo upendo wako tuutukuze kuliko mvinyo!

Wanakupenda kwelikweli.

5Mimi ni mweusi, lakini ninapendeza,

ninyi wanawake wa Yerusalemu!

Nafanana na mahema ya Kedari, tena na mazulia ya Salomo.

6Msinionee kwa kuwa mweusimweusi! Ni jua lililonichoma.

Wana wa mama yangu walinikasirikia,

maana waliniweka kuwa mlinzi wa mashamba ya mizabibu,

lakini hata shamba langu la mizabibu sikulilinda.

7Niambie wewe, mpendwa wa roho yangu: Unalishia wapi?

Tena ni wapi, unapowapumzishia kondoo, jua likiwa kali?

Mbona niwe kama mwenye kutangatanga penye makundi ya wenzako?

8“Usipopajua mwenyewe uliye mzuri kuliko wanawake wengine,

toka tu na kuzifuata nyayo za kondoo,

kavichunge vitoto vyako vya mbuzi matuoni kwa wachungaji!

9Ninakufananisha wewe, mpenzi wangu,

na farasi avutaye gari la Farao.

10Mashavu yako hupendeza kwa kili za nywele,

nayo shingo yako yenye ushanga.

11Na tukutengenezee vikufu vya dhahabu

vyenye vifungo vya fedha.

12Mfalme akiwa anakaa mezani pake,

manukato yangu ya narada hutoa mnuko wao mzuri.”

13Mpendwa wangu ni kifuko cha manemane

kikaacho katikati ya maziwa yangu.

14Mpendwa wangu ni kichala cha mhina

kitokacho mizabibuni kwenye Engedi.

15Nikikutazama, mpenzi wangu, u mwanamke mzuri,

“u mwanamke mzuri kweli mwenye macho kama ya hua.”

16Wewe nawe, mpendwa wangu, u kijana mzuri, unapendeza kweli.

Malalo yetu ni majani mabichi.

17“Boriti za nyumba yetu ni miangati,

mbau zetu za kuzifunika kuta ni mvinje.”

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania