Wimbo mkuu 2

Wimbo mkuu 2

Mwanamke anamtunukia mpendwa wake.

1Mimi ni ua la uwago wa Saroni, ni nyinyoro ya mabondeni.

2“Kama ua lilivyo katikati ya miiba,

ndivyo, mpenzi wangu alivyo katikati ya wanawali.”

3Kama mchungwa ulivyo katikati ya miti ya msituni,

ndivyo, mpendwa wangu alivyo katikati ya vijana.

Kwa kumtunukia nilikaa kivulini kwake;

tunda lake ni tamu sana, nikilila.

4Akaniingiza nyumbani, wanyweamo mvinyo,

nayo bendera yake iliyokuwa juu yangu, ni upendo.

5Nitieni nguvu kwa maandazi ya zabibu, kaniinueni kwa machungwa!

Kwani mimi ni mgonjwa kwa kupenda sana.

6Mkono wake wa kushoto uko chini ya kichwa changu,

nao wa kuume unanikumbatia.

7“Nawaapisha ninyi, wanawake wa Yerusalemu,

nikiwataja paa na kulungu wake walioko porini,

msimwamshe, wala msimhangaishe yeye ninayempenda,

ila mwacheni tu, mpaka atakapopendezwa mwenyewe!”

8Iko sauti ya mpendwa wangu, naisikia, anakuja

akiruka milimani, akichezacheza vilimani.

9Mpendwa wangu anafanana na paa mume au na kijana wa kulungu.

Mtazame! Yuko akisimama nyuma ya kitalu chetu,

akichungulia madirishani, akaonekana penye vyuma vyao.

10Mpendwa wangu ananiita na kuniambia:

“Inuka, mpenzi wangu mzuri, uje hapa!

11Kwani tazama! Kipupwe kimepita,

mvua nayo ikakoma, ikaenda zake.

12Maua yanaonekana katika nchi, siku za kuimba zimetimia,

sauti za hua zinasikilika katika nchi yetu.

13Mkuyu unaanza kuziivisha kuyu zake changa,

nayo mizabibu inachanua maua yanukayo vema;

inuka, mpenzi wangu mzuri, uje hapa!

14Hua yangu hapo ngomeni penye mwamba, ulijificha magengeni,

nipe kuuona uso wako, nipe kuisikia nayo sauti yako!

Kwani sauti yako ni tamu, nao uso wako unapendeza.

15Tukamatieni nyegere, nyegere wale wadogo!

Maana huiharibu mizabibu, nayo mizabibu yetu inachanua.”

16Mpendwa wangu ni wangu, nami ni wake yeye

alishaye penye nyinyoro.

17Mpaka jua la mchana lipunguke ukali, vivuli vikijiendea mbiombio,

geuka, mpendwa wangu, uruke kama paa au kijana wa kulungu,

milimani kwenye makorongo!

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania