Tito 2

Tito 2

Kuwaonya waume na wanawake na watumwa.

1Lakini wewe sema yapatanayo na ufundisho utupao uzima![#1 Tim. 6:3; 2 Tim. 1:13.]

2Waume wazee sharti wawe watu wasiokunywa kileo, wapewe macheo, wawe werevu wa kweli, wajipatie uzima kwa kumtegemea Mungu na kwa kupendana na kwa kuvumilia kwao![#1 Tim. 5:1-16.]

3Vivyo hivyo wanawake wazee nao sharti wafanye mwenendo uwapasao walio watakatifu! Wasisengenye wala wasiwe watumwa wa unywaji wa pombe nyingi, ila wenye kufundisha wengine yaliyo mazuri,[#1 Tim. 3:11.]

4wapate kuwaerevusha wanawake walio vijana bado, wawapende waume na watoto wao!

5Hivyo nao wake vijana watakuwa werevu wa kweli, wang'avu, wenye kutengeneza nyumba zao vizuri, wenye wema na wenye kuwatii waume wao, Neno la Mungu lisibezwe.[#Ef. 5:22.]

6Lakini vilevile waambie vijana waume na kuwakanya, waerevuke kweli!

7Katika mambo yote ujiweke mwenyewe kuwawia kielezo cha kujifundishia matendo mazuri! Wafundishe kujiangalia miili, waipe macheo yaipasayo![#1 Tim. 4:12; 1 Petr. 5:3.]

8Litangaze Neno litupalo uzima lisilobishika, mpingani aingiwe na soni, asiweze kusema neno ovu lo lote la kutusuta![#1 Petr. 2:15.]

9Walio watumwa waambie, wawatii mabwana zao, wawapendeze katika mambo yote, wasiwe wabishi,[#Ef. 6:5-6; 1 Tim. 6:1-2; 1 Petr. 2:18.]

10wasiibe ila wajionyeshe kuwa wenye welekevu na wema wote, matendo yao yote yawe mapambo ya ufundisho wa mwokozi na Mungu wetu![#Tit. 1:3.]

Mema ya Mungu yenye kuleta wokovu.

11*Kwani mema yake Mungu, ayagawiayo watu wote ya kuwaokoa, yametokea waziwazi,

12nayo hutuonya, tuuvunje mwenendo wa kimizimu, tusizifuate tamaa za humu ulimwenguni, ila siku hizi za sasa za kuishi duniani tuwe wenye werevu wa kweli na wenye wongofu na wenye kumcha Mungu.[#Ef. 1:4.]

13Kisha tuchungue, kingojeo chetu cha kutushangiliza kitakavyotimia, utukufu wa Mungu wetu mkuu na wa mwokozi wetu Kristo Yesu utakapotokea.[#1 Kor. 1:7; Fil. 3:20.]

14Yeye ndiye aliyejitoa mwenyewe kwa ajili yetu kuwa kole ya kuyalipa mapotovu yote, ajipatie watu wang'avu watakaokuwa wake wenye bidii ya kufanya kazi nzuri.*[#Ez. 37:23; Gal. 1:4; Ef. 2:10; 1 Tim. 2:6.]

15Hayo yaseme na kuwaonya na kuwashinda wakosaji kwa nguvu zote! Mtu asikubeze[#1 Tim. 4:12.]

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania