Sefania 1

Sefania 1

Siku ya makali ya Bwana.

1Hili ndilo neno la Bwana lililomjia Sefania, mwana wa Kusi, mwana wa Gedalia, mwana wa Amaria, mwana wa Hizikia, siku zile, Yosia, mwana wa Amoni, alipokuwa mfalme wa Yuda.[#Yer. 1:2.]

2Ndivyo, asemavyo Bwana:

Nitayakusanya kabisa yote pia na kuyaondoa juu ya nchi:

3nitawakusanya na kuwaondoa watu na nyama, nao ndege wa angani,

nao samaki wa baharini nitawakusanya na kuwaondoa,

nayo makwazo pamoja nao wasiomcha Mungu,

niwatoweshe watu juu ya nchi hii.

Ndivyo, asemavyo Bwana:

4Nitaukunjua mkono wangu, uwakamate Wayuda

nao wote wakaao Yerusalemu;

masao yote ya Baali nitayatowesha mahali hapa,

majina yao watangazaji pamoja nayo ya watambikaji.

5Nao wanaokitambikia kikosi cha mbinguni juu ya paa

pamoja nao wanaomtambikia Bwana juujuu,

kwani huapa na kumtaja Yeye, tena huapa na kumtaja mfalme wao.

6Nao waliorudi nyuma na kumwacha Bwana,

hawamtafuti Bwana, wala hawamchungulii.

7Nyamazeni kimya usoni pa Bwana Mungu!

Kwani siku ya Bwana iko karibu,

kwani Bwana amekwisha kulilinganya tambiko,

akawaeua walioalikwa naye.

8Itakuwa siku ya tambiko la Bwana, ndipo, nitakapowapatiliza

wakuu nao wana wa mfalme, nao wote waliojivika mavazi mageni.

9Siku hiyo ndipo, nitakapowapatiliza wote warukao juu ya kizingiti,

nao wanaoijaza Nyumba ya Bwana, wao wakorofi na wadanganyifu.

Ndivyo, asemavyo Bwana:

10Siku hiyo itakuwa, makelele yasikilike penye Lango la Samaki,

na vilio katika mitaa ya nje na uvumi wa maanguko makuu vilimani.

11lieni, mkaao penye barabara ya Vinu!

Kwani kabila zima la wachuuzi litakuwa limeangamizwa,

watatoweshwa wote wachukuao fedha!

12Siku hizo itakuwa, nitakapochunguzia Yerusalemu kwa mienge ya moto,

niwavumbue wajikaliao tu penye shimbi za mvinyo zao na kusema mioyoni mwao:

Bwana hafanyi wala mema wala mabaya.

13Mali zao zote zitakuwa mateka,

nazo nyumba zao zitakuwa mahame;

watajenga nyumba, lakini hawatakunywa mvinyo zao.

14Siku ya Bwana iliyo kuu iko karibu,

iko karibu kweli, inataka kutimia upesi.

Uvumi wa siku ya Bwana utakaposikilika,

ndipo, naye mnguvu atakapolia kwa uchungu.

15Siku hiyo ni siku ya machafuko,

ni siku ya kusongeka na ya kubanwa,

ni siku ya uangamivu na ya upotevu,

ni siku yenye giza na weusi,

ni siku yenye mawingu meusi kama ya usiku,

16ni siku ya kupiga mabaragumu na yowe

ya kutisha miji yenye maboma na minara mirefu.

17Ndipo, nitakapowaogopesha watu, wajiendee kama vipofu,

kwani wamemkosea Bwana!

Nazo damu zao zitamwagwa kama mavumbi,

nazo nyama za miili yao zitatupwa kama mavi.

18Hata fedha zao na dhahabu zao hazitaweza kuwaponya

siku hiyo ya machafuko ya Bwana;

katika moto wa wivu wake

nchi hii yote nzima itateketea,

kwani wote wakaao katika nchi hii atawaishiliza wote pia,

wakiguiwa na kituko kwa mara moja.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania