1 Mambo ya Nyakati 18

1 Mambo ya Nyakati 18

Milki ya Daudi yaimarika na kupanuka

1Ikawa baadaye, Daudi akawapiga Wafilisti, akawashinda, akautwaa Gathi na vijiji vyake mikononi mwa Wafilisti.[#2 Sam 8:1]

2Akapiga Moabu; na hao Wamoabi wakawa watumishi wa Daudi wakaleta zawadi.[#Hes 24:17]

3Tena Daudi akampiga Hadadezeri, mfalme wa Soba, mpaka Hamathi, alipokwenda kujisimamishia mnara wa ukumbusho kwenye mto wa Frati.[#2 Sam 8:3; Mwa 15:18; Kum 11:24]

4Daudi akampokonya magari elfu moja, na wapanda farasi elfu saba, na askari waendao kwa miguu elfu ishirini; Daudi akawakata mshipa farasi wote wa magari, ila wa magari mia moja akawaweka.[#2 Sam 8:4]

5Na Washami wa Dameski walipokuja wamsaidie Hadadezeri, mfalme wa Soba, Daudi akapiga katika hao Washami watu elfu ishirini na mbili.

6Ndipo Daudi akaweka ngome katika Shamu ya Dameski; nao Washami wakawa watumwa wa Daudi, wakaleta zawadi. Naye BWANA akampa Daudi kushinda kila alikokwenda.[#1 Nya 17:8; Zab 91:14; 121:8; Mit 21:31]

7Tena Daudi akazitwaa ngao za dhahabu zilizovaliwa na watumishi wa Hadadezeri akazileta Yerusalemu.

8Tena toka Tibhathi, na toka Berothai, miji ya Hadadezeri, Daudi akatwaa shaba nyingi mno, aliyoitumia Sulemani katika kutengeneza lile birika la shaba, na zile nguzo, na vile vyombo vya shaba.[#1 Fal 7:15; 2 Nya 4:12-16]

9Hata aliposikia Tou, mfalme wa Hamathi, ya kuwa Daudi amewapiga jeshi lote la Hadadezeri, mfalme wa Soba,[#2 Sam 8:9]

10akamtuma mwanawe Hadoramu kwa mfalme Daudi, ili kumsalimia, na kumbarikia, kwa sababu alikuwa amepigana na Hadadezeri, na kumpiga; kwa maana Hadadezeri alikuwa amepigana vita juu ya Tou; naye akaleta vyombo vya dhahabu, na fedha, na shaba, vya namna zote.[#2 Sam 8:10]

11Hivi pia mfalme Daudi akavifanya wakfu kwa BWANA, pamoja na hiyo fedha na dhahabu, aliyoteka nyara kwa mataifa yote; kwa Edomu, na kwa Moabu, na kwa wana wa Amoni, na kwa Wafilisti, na kwa Amaleki.

12Tena Abishai, mwana wa Seruya, akawaua Waedomi elfu kumi na nane katika Bonde la Chumvi.[#2 Sam 7:13; 2 Fal 14:7; 2 Nya 25:11]

13Akaweka ngome katika Edomu; na Waedomi wote wakawa watumishi wa Daudi. Naye BWANA akampa Daudi ushindi, kila alikokwenda.[#Mwa 27:29; Hes 24:18; 1 Sam 10:5; 13:3; 14:1]

Utawala wa Daudi

14Basi Daudi akawatawala Waisraeli wote; akawafanyia hukumu na haki watu wake wote.

15Na Yoabu mwana wa Seruya akawa mkuu wa jeshi; na Yehoshafati mwana wa Ahiludi mwenye kuandika tarehe.[#18:15 Au, mkumbushi.]

16Na Sadoki mwana wa Ahitubu, na Ahimeleki mwana wa Abiathari, walikuwa makuhani; na Shausha mwandishi;

17na Benaya mwana wa Yehoyada alikuwa mkuu wa Wakerethi na Wapelethi; na wana wa Daudi walikuwa mofisa wakuu wa mfalme.[#2 Sam 8:18]

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya