1 Mambo ya Nyakati 20

1 Mambo ya Nyakati 20

Kuzingirwa na kutekwa kwa Raba

1Hata ikawa, mwanzo wa mwaka mpya, wakati watokapo wafalme kwenda vitani, Yoabu akawaongoza mashujaa wa jeshi, akaiteka nyara nchi ya wana wa Amoni, akaja akauzingira Raba. Lakini Daudi akakaa Yerusalemu. Naye Yoabu akaupiga Raba akauangamiza.[#2 Sam 11:1; 1 Fal 20:22; 2 Nya 36:10; Mhu 3:8; 2 Sam 12:26; Yer 49:2; Eze 21:20]

2Kisha Daudi akatwaa taji la Milkomu toka kichwani pake, akaona ya kwamba uzani wake ni talanta ya dhahabu, na kulikuwa na vito vya thamani ndani yake; akavikwa Daudi kichwani; akazitoa nyara za mji, nyingi sana.[#2 Sam 12:30,31; #20:2 Katika makala zingine ni mfalme wao.]

3Na hao watu waliokuwamo akawatoa, akawawafanyisha kazi kwa misumeno, na kwa sululu za chuma, na kwa mashoka. Ndivyo alivyofanya Daudi kwa miji yote ya wana wa Amoni. Nao wakarudi Yerusalemu Daudi na watu wote.

Kushindwa kwa Wafilisti

4Ikawa baada ya hayo, kulitokea vita na Wafilisti huko Gezeri; ndipo Sibekai, Mhushathi, alipomwua Safu, mmojawapo wa Warefai; nao Wafilisti wakashindwa.[#20:4 Au, wana wa jitu.; #20:4 Katika Kiebrania hakuna Wafilisti.]

5Kulikuwa na vita tena na Wafilisti; na Elhanani, mwana wa Yairi akamwua Lahmi nduguye Goliathi, Mgiti, ambaye mti wa mkuki wake ulikuwa kama mti wa mfumaji.[#20:5 Au, Mbethlehemi akamwua nduguye Goliathi.]

6Kulikuwa na vita tena huko Gathi; ambapo palikuwa na mtu mrefu sana, mwenye vidole vya mikono na miguu ishirini na vinne, kila mguu sita, na kila mkono sita; naye alizaliwa na Mrefai.[#20:6,8 Au, huyu jitu.]

7Naye huyo alipowatukana Israeli, Yonathani, mwana wa Shama, nduguye Daudi, akamwua.

8Hao walizaliwa kwake huyo Mrefai wa Gathi, nao wakaanguka kwa mkono wa Daudi, na kwa mkono wa watumishi wake.[#20:6,8 Au, huyu jitu.]

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya