The chat will start when you send the first message.
1Kwa maana, ndugu zangu, sipendi mkose kufahamu ya kuwa baba zetu walikuwa wote chini ya wingu; wote wakapita kati ya bahari;[#Kut 13:21-22; 14:22-29]
2wote wakabatizwa wawe wa Musa katika wingu na katika bahari;
3wote wakala chakula kile kile cha roho;[#Kut 16:4,35; Kum 8:3]
4wote wakanywa kinywaji kile kile cha roho; kwa maana waliunywea mwamba wa roho uliowafuata; na mwamba ule ulikuwa ni Kristo.[#Kut 17:6; Hes 20:11]
5Lakini wengi sana katika wao, Mungu hakupendezwa nao; maana waliangamizwa jangwani.[#Hes 14:16,23,29-30]
6Basi mambo hayo yalikuwa mifano kwetu, kusudi sisi tusiwe watu wa kutamani mabaya, kama wale nao walivyotamani.[#Hes 11:4,34]
7Wala msiwe waabudu sanamu, kama wengine wao walivyokuwa; kama ilivyoandikwa, Watu waliketi kula na kunywa, kisha wakasimama wacheze.[#Kut 32:6]
8Wala msifanye uasherati, kama wengine wao walivyofanya, wakaanguka siku moja watu elfu ishirini na tatu.[#Hes 25:1-18]
9Wala tusimjaribu Bwana, kama wengine wao walivyomjaribu, wakauawa na nyoka.[#Hes 21:5-6]
10Wala msinung'unike, kama wengine wao walivyonung'unika, wakauawa na mharibifu.[#Hes 16:41-49; 14:2,36; Ebr 3:11,17]
11Basi mambo hayo yaliwapata wao kwa jinsi ya mifano, yakaandikwa ili kutuonya sisi, tuliofikiwa na miisho ya nyakati.[#1 Pet 4:7]
12Kwa hiyo anayejidhania kuwa amesimama na aangalie asianguke.
13Jaribu halikuwapata ninyi, isipokuwa lililo kawaida ya wanadamu; ila Mungu ni mwaminifu; ambaye hatawaacha mjaribiwe kupita muwezavyo; lakini pamoja na lile jaribu atafanya na mlango wa kutokea, ili muweze kustahimili.
14Kwa ajili ya hayo, wapenzi wangu, ikimbieni ibada ya sanamu.[#1 Yoh 5:21]
15Nasema kama na watu wenye akili; lifikirini ninyi ninenalo.
16Kikombe kile cha baraka tukibarikicho, je! Si ushirika wa damu ya Kristo? Mkate ule tuumegao, si ushirika wa mwili wa Kristo?[#Mt 26:26-28; Mk 14:22-24; Lk 22:19-20; Mdo 2:42]
17Kwa kuwa mkate ni mmoja, sisi tulio wengi tu mwili mmoja; kwa maana sisi sote twapokea sehemu ya ule mkate mmoja.[#1 Kor 12:27; Rum 12:5]
18Waangalieni hao Waisraeli walivyokuwa kwa jinsi ya mwili; wale wazilao dhabihu, je! Hawana shirika na madhabahu?[#Law 7:6,15]
19Basi niseme nini? Ya kwamba kile kilichotolewa sadaka kwa sanamu ni kitu? Au ya kwamba sanamu ni kitu?[#1 Kor 8:4]
20Sivyo, lakini vitu vile wavitoavyo sadaka wavitoa kwa mashetani, wala si kwa Mungu; nami sipendi ninyi kushirikiana na mashetani. Hamwezi kunywea kikombe cha Bwana na kikombe cha mashetani.[#Kum 32:17; Law 17:7; Zab 106:37; Ufu 9:20]
21Hamwezi kushirikiana katika meza ya Bwana na katika meza ya mashetani.[#2 Kor 6:15,16; Mal 1:7,12]
22Au twamtia Bwana wivu? Je! Tuna nguvu zaidi ya yeye?[#Kum 32:21]
23Vitu vyote ni halali; bali si vitu vyote vifaavyo. Vitu vyote ni halali; bali si vitu vyote vijengavyo.[#1 Kor 6:12]
24Mtu asitafute faida yake mwenyewe, bali ya mwenzake.[#Rum 15:2]
25Kila kitu kiuzwacho sokoni kuleni, bila kuulizauliza, kwa ajili ya dhamiri;[#1 Kor 14:2-10,22]
26maana, Dunia ni mali ya Bwana na vyote viijazavyo.[#Zab 24:1]
27Na mtu asiyeamini akiwaalika, nanyi mnataka kwenda, kuleni kila kitu kiwekwacho mbele yenu bila kuulizauliza, kwa ajili ya dhamiri.[#Lk 10:8]
28Lakini mtu akiwaambia, Kitu hiki kimetolewa kiwe sadaka, msile, kwa ajili yake yeye aliyewaambia, na kwa ajili ya dhamiri.[#1 Kor 8:7]
29Nasema, dhamiri, lakini si yako, bali ya yule mwingine. Maana kwa nini uhuru wangu uhukumiwe na dhamiri ya mtu mwingine?
30Ikiwa mimi natumia sehemu yangu kwa shukrani, kwa nini nitukanwe, kwa ajili ya kitu nikishukuriacho?[#1 Tim 4:4]
31Basi, mlapo, au mnywapo, au mtendapo neno lolote, fanyeni yote kwa utukufu wa Mungu.[#Kol 3:17]
32Msiwakoseshe Wayahudi wala Wagiriki wala kanisa la Mungu,[#Rum 14:13]
33vile vile kama mimi niwapendezavyo watu wote katika mambo yote, nisitake faida yangu mwenyewe, ila faida yao walio wengi, wapate kuokolewa.[#1 Kor 9:20-22]