The chat will start when you send the first message.
1Basi Eliya Mtishbi, wa wageni wa Gileadi, akamwambia Ahabu, Kama BWANA, Mungu wa Israeli, aishivyo, ambaye ninasimama mbele zake, hakutakuwa na umande wala mvua miaka hii, ila kwa neno langu.[#Lk 1:17; 4:25; 2 Fal 3:14; Kum 10:8; Yak 5:17]
2Neno la BWANA likamjia, kusema,
3Ondoka hapa, geuka, uende upande wa mashariki, ujifiche karibu na kijito cha Kerithi kinachokabili Yordani.
4Itakuwa utakunywa maji ya kile kijito; nami nimewaamuru kunguru wakulishe huko.[#Zab 37:3; Isa 33:15]
5Basi akaenda akafanya kama alivyosema BWANA; kwa kuwa alikwenda akakaa karibu na kijito cha Kerithi, kinachokabili Yordani.
6Kunguru wakamletea mkate na nyama asubuhi, na mkate na nyama jioni, akanywa maji ya kile kijito.
7Ikawa, baada ya siku kupita, kile kijito kikakatika, kwa sababu mvua haikunyesha katika nchi.
8Neno la BWANA likamjia, kusema,
9Ondoka, uende Sarepta, ulio mji wa Sidoni, ukae huko. Tazama, nimemwagiza mwanamke mjane wa huko akulishe.[#Oba 1:20; Lk 4:26]
10Basi, akaondoka, akaenda Sarepta; hata alipofika langoni pa mji, kumbe! Mwanamke mjane alikuwako akiokota kuni; akamwita, akamwambia, Niletee, nakuomba, maji kidogo chomboni nipate kunywa.[#Mwa 24:7; Zab 24:1; Isa 33:16; Yn 4:7; Ebr 11:37]
11Alipokuwa akienda kuleta, akamwita akasema, Niletee, nakuomba, kipande cha mkate mkononi mwako.
12Naye akasema, Kama BWANA, Mungu wako, aishivyo, sina mkate, ila konzi ya unga katika pipa, na mafuta kidogo katika chupa; nami ninaokota kuni mbili ili niingie nijipikie mwenyewe na mwanangu, tule kisha tufe.[#Mwa 18:6; 21:15,16]
13Eliya akamwambia, Usiogope; nenda ukafanye kama ulivyosema; lakini unifanyie kwanza mkate mdogo ukaniletee; kisha ujitengenezee na mwanao.[#Mwa 22:1,2; 1 Pet 1:7]
14Kwa kuwa BWANA, Mungu wa Israeli, asema hivi, Lile pipa la unga halitapunguka, wala ile chupa ya mafuta haitaisha, hata siku ile BWANA atakapoleta mvua juu ya nchi.[#Zab 84:7-10,12; 34:11; 1 Tim 4:8; Flp 4:19]
15Basi akaenda, akafanya kama alivyosema Eliya; na yeye mwenyewe, na Eliya, na nyumba yake, wakala siku nyingi.[#2 Nya 20:20; Mt 10:41,42; 20:28; Ebr 11:8]
16Lile pipa la unga halikupunguka, wala ile chupa ya mafuta haikuisha, sawasawa na neno la BWANA alilolinena kwa kinywa cha Eliya.[#Kum 15:10; Mit 11:24]
17Ikawa, baada ya hayo, mwana wake yule mwanamke, bibi wa nyumba ile, akaugua; ugonjwa wake ukazidi hata akawa hana pumzi tena.
18Akamwambia Eliya, Nina nini nawe, Ee mtu wa Mungu? Je! Umenijia ili dhambi yangu ikumbukwe, ukamwue mwanangu?[#2 Sam 16:10; Lk 4:34; 5:8; Yn 2:4]
19Akamwambia, Nipe mwanao. Akamtoa katika kifua chake, akamchukua juu chumbani mle alimokaa mwenyewe, akamlaza kitandani pake.
20Akamwomba BWANA, akanena, Ee BWANA, Mungu wangu, je! Umemtenda mabaya mjane huyu ninayekaa kwake hata kumwua mwanawe?[#Kut 15:25; 17:4; Hes 11:11; 1 Sam 7:8; 1 Fal 18:36,37; Flp 4:6; Yak 5:13,16]
21Akajinyosha juu ya mtoto mara tatu, akamwomba BWANA, akanena, Ee BWANA, Mungu wangu, nakusihi, roho ya mtoto huyu imrudie ndani yake tena.[#2 Fal 4:34,35; Mdo 20:10]
22BWANA akaisikia sauti ya Eliya; na roho ya mtoto ikamrudia, akafufuka.[#Zab 65:2; 66:19; Mit 15:8,29; Mt 21:22; Lk 11:9,10; 1 Yoh 3:22; 5:14; Kum 32:39; Lk 7:14; Mdo 20:10,12; Ebr 11:35]
23Eliya akamtwaa mtoto, akamchukua toka ghorofani mpaka chini ya nyumba ile, akampa mama yake. Eliya akanena, Tazama, mwanao yu hai.
24Mwanamke akamwambia Eliya, Sasa najua ya kuwa wewe ndiwe mtu wa Mungu, na ya kuwa neno la BWANA kinywani mwako ni kweli.[#Yn 3:2; 16:30]