1 Wafalme 19

1 Wafalme 19

Eliya amkimbia Yezebeli

1Basi, Ahabu akamwambia Yezebeli habari ya mambo yote aliyoyafanya Eliya, na jinsi alivyowaua manabii wote kwa upanga.[#1 Fal 18:40]

2Ndipo Yezebeli akampelekea Eliya mjumbe, kusema, Miungu wanifanyie hivyo na kuzidi, nisipokufanya roho yako kesho, panapo wakati huu, kama roho ya mmojawapo wa hao.[#Rut 1:17; 1 Fal 2:23; 20:10; 2 Fal 6:31; Mit 27:1]

3Naye alipoona hayo, aliondoka, akaenda aihifadhi roho yake, akafika Beer-sheba, mji wa Yuda, akamwacha mtumishi wake huko.

4Lakini yeye mwenyewe akaendelea katika jangwa mwendo wa siku moja, akaenda akaketi chini ya mretemu. Akajiombea roho yake afe, akasema, Yatosha; sasa, Ee BWANA, uiondoe roho yangu; kwa kuwa mimi si mwema kuliko baba zangu.[#Hes 11:15; Yer 26:14-18; Yon 4:3-8; Flp 1:21-24]

5Naye akajinyosha akalala chini ya mretemu; na tazama, malaika akamgusa, akamwambia, Inuka, ule.[#Zab 34:7; Mdo 12:7; Ebr 1:14]

6Akatazama, kumbe! Pana mkate umeokwa juu ya makaa, na gudulia la maji, kichwani pake. Akala, akanywa, akajinyosha tena.

7Malaika wa BWANA akamwendea mara ya pili, akamgusa, akasema, Inuka, ule; maana safari hii ni kubwa mno kwako.

8Akainuka, akala, akanywa, akaenda katika nguvu za chakula hicho siku arubaini mchana na usiku hata akafika Horebu, mlima wa Mungu.[#Kut 24:18; 34:28; Kum 9:9,18; Mt 4:2; Lk 4:2; Kut 3:1]

9Akafika kunako pango, akalala ndani yake. Na tazama, neno la BWANA likamjia, naye akamwambia, Unafanya nini hapa, Eliya?[#Kut 33:21; Ebr 11:38]

10Akasema, Nimeona wivu mwingi kwa ajili ya BWANA Mungu wa majeshi; kwa kuwa wana wa Israeli wameyaacha maagano yako, na kuzivunja madhabahu zako, na kuwaua manabii wako kwa upanga; nami nimesalia, mimi peke yangu; nao wanitafuta roho yangu, waiondoe.[#Rum 11:3; Kut 20:5; Hes 20:5,11; Zab 69:9; 119:139; 1 Fal 18:4,22; Mt 23:31-35]

Mungu amtokea Eliya Mlimani Horebu

11Akasema, Toka, usimame mlimani mbele za BWANA. Na tazama, BWANA akapita; upepo mwingi wa nguvu ukaipasua milima, ukaivunjavunja miamba mbele za BWANA; lakini BWANA hakuwamo katika upepo ule; na baada ya upepo, tetemeko la nchi; lakini BWANA hakuwamo katika lile tetemeko la nchi;[#Kut 24:12; Eze 1:4; 37:7]

12na baada ya tetemeko la nchi kukawa na moto; lakini BWANA hakuwamo katika moto ule; na baada ya moto sauti ndogo, ya utulivu.[#Hes 14:18; Neh 9:17; Ayu 4:16; Zab 86:15; 145:8; Yak 5:11]

13Ikawa, Eliya alipoisikia, alijifunika uso wake katika mavazi yake, akatoka, akasimama mlangoni mwa pango. Na tazama, sauti ikamjia, kusema, Unafanya nini hapa, Eliya?[#Kut 3:6; Isa 6:2]

14Akasema, Nimeona wivu mwingi kwa ajili ya BWANA, Mungu wa majeshi; kwa kuwa wana wa Israeli wameyaacha maagano yako, na kuzivunja madhabahu zako, na kuwaua manabii wako kwa upanga; nami nimesalia, mimi peke yangu; nao wanitafuta roho yangu waiondoe.

15BWANA akamwambia, Nenda, urudi njia ya jangwa la Dameski; ukifika, mtie mafuta Hazaeli awe mfalme wa Shamu.[#2 Fal 8:12,13]

16Na Yehu mwana wa Nimshi mtie mafuta awe mfalme wa Israeli; na Elisha mwana wa Shafati wa Abel-Mehola mtie mafuta awe nabii mahali pako.[#2 Fal 9:1; Lk 4:27]

17Na itakuwa atakayeokoka na upanga wa Hazaeli, Yehu atamwua; na atakayeokoka na upanga wa Yehu, Elisha atamwua.[#2 Fal 8:12; 9:14; 10:6; 13:3; Amo 2:14; 2 Fal 2:23,24; Isa 11:4; Hos 6:5; Ufu 19:21]

18Pamoja na hayo nitajisazia katika Israeli watu elfu saba, kila goti lisilomwinamia Baali, na kila kinywa kisichombusu.[#Isa 1:9; Eze 6:8; 14:22; Yoe 2:32; Rum 11:4; Ayu 31:27; Hos 13:2]

Elisha kuwa mwanafunzi wa Eliya

19Basi, akaondoka huko, akamkuta Elisha mwana wa Shafati, aliyekuwa akilima, mwenye jozi za ng'ombe kumi na mbili mbele yake, na yeye mwenyewe alikuwa pamoja na lile la kumi na mbili. Eliya akapita karibu naye, akatupa vazi lake juu yake.

20Naye akawaacha ng'ombe, akamfuata Eliya mbio, akasema, Nipe ruhusa, nakuomba, nimbusu baba yangu na mama yangu, kisha mimi nitakufuata. Akamwambia, Nenda, urudi; ni nini niliyokutendea?

21Akarudi akiacha kumfuata, akatwaa lile jozi la ng'ombe, akawachinja, akatokosa nyama zao kwa ile miti ya ng'ombe, akawapa watu, wakala. Kisha akainuka, akamfuata Eliya, akamhudumia.[#2 Sam 24:22; Mt 4:18-22; Lk 5:27,28; Kut 24:13]

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya