1 Petro 4

1 Petro 4

Mawakili wema na neema ya Mungu

1Basi kwa kuwa Kristo aliteswa katika mwili wake, ninyi nanyi jivikeni silaha ya nia ile ile; kwa maana yeye aliyeteswa katika mwili ameachana na dhambi.[#Rum 6:2,7]

2Tangu sasa msiendelee kuishi katika tamaa za wanadamu, bali katika mapenzi ya Mungu, wakati wenu uliobaki wa kukaa hapa duniani.[#1 Yoh 2:16,17]

3Maana wakati wa maisha yetu uliopita watosha kwa kutenda mapenzi ya Mataifa; kuishi katika uzinzi, tamaa, ulevi, na karamu za kula na kunywa vileo kupindukia, na ibada haramu ya sanamu;[#Efe 2:2,3; Tit 3:3]

4mambo ambayo wao huona kuwa ni ajabu ya ninyi kutokwenda mbio pamoja nao katika ufisadi ule ule usio na kiasi, wakiwatukana.

5Nao watatoa hesabu kwake yeye aliye tayari kuwahukumu walio hai na waliokufa.[#Mdo 10:42; 2 Tim 4:1; Rum 14:9,10]

6Maana kwa ajili hiyo hata hao waliokufa walihubiriwa Injili, ili kwamba wahukumiwe katika mwili kama wahukumiwavyo wanadamu; bali wawe hai katika roho kama Mungu alivyo hai.[#1 Pet 3:19; Rum 8:10; 1 Kor 5:5]

7Lakini mwisho wa mambo yote umekaribia; basi, iweni na akili, mkeshe katika sala.[#1 Kor 10:11; 1 Yoh 2:18]

8Zaidi ya yote iweni na bidii kubwa katika kupendana; kwa sababu upendano husitiri wingi wa dhambi.[#Mit 10:12; 1 Pet 1:22; Yak 5:20; 1 Kor 13:7]

9Mkaribishane ninyi kwa ninyi, pasipo kunung'unika;[#Ebr 13:2]

10kila mmoja kwa kadiri alivyoipokea karama, itumieni kwa kuhudumiana; kama mawakili wema wa neema mbalimbali za Mungu.[#Lk 12:42]

11Mtu akisema, na aseme kama asemaye maneno halisi ya Mungu; mtu akihudumu, na ahudumu kwa nguvu anazojaliwa na Mungu; ili Mungu atukuzwe katika mambo yote kwa Yesu Kristo. Utukufu na uweza una yeye hata milele na milele. Amina.[#Rum 3:2; 12:7; 1 Kor 10:31]

Kuteseka kama Mkristo

12Wapenzi, msione kuwa ni ajabu ule msiba ulio kati yenu, unaowapata kama moto ili kuwajaribu, kana kwamba ni kitu kigeni kiwapatacho.[#1 Pet 1:6,7]

13Lakini kama mnavyoyashiriki mateso ya Kristo, furahini; ili pia katika ufunuo wa utukufu wake mfurahi kwa shangwe.[#Mdo 5:41; Yak 1:2; Rum 8:17; 2 Tim 2:12]

14Mkilaumiwa kwa ajili ya jina la Kristo ni heri yenu; kwa kuwa Roho wa utukufu na wa Mungu anawakalia.[#1 Pet 2:20; Isa 11:2; Zab 89:50,51]

15Lakini pasiwe na hata mmoja wenu atakayeteseka kwa kuwa mwuaji, mwizi, mhalifu au hata mfitini.

16Lakini ikiwa mtu yeyote miongoni mwenu anateseka kwa sababu ni Mkristo, asione haya, bali amtukuze Mungu maana ana jina hili.[#Mdo 11:26; Flp 1:20]

17Kwa maana wakati umefika wa hukumu kuanza katika nyumba ya Mungu; na ikianza kwetu sisi, mwisho wao wasioitii Injili ya Mungu utakuwaje?[#Eze 9:6; Yer 25:29; 2 The 1:8]

18Na mwenye haki akiokoka kwa shida, yule asiyemcha Mungu na mwenye dhambi ataonekana wapi?[#Mit 11:31; Lk 23:31]

19Basi wao wateswao kwa mapenzi ya Mungu na wamwekee amana roho zao, katika kutenda mema, kama kwa Muumba mwaminifu.[#Zab 31:5]

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya