The chat will start when you send the first message.
1Maana ninyi wenyewe, ndugu, mnakujua kuingia kwetu kwenu, ya kwamba hakukuwa bure;[#1 The 1:5,9; 2 The 3:7]
2ingawa tuliteswa na kutukanwa, katika Filipi kama mjuavyo, tulithubutu katika Mungu kuinena Injili ya Mungu kwenu, kwa kuishindania sana.[#Mdo 16:19-24; 17:1-9]
3Kwa maana maonyo yetu siyo ya ukosefu, wala ya uchafu, wala ya hila;
4bali kama vile tulivyopata kibali kwa Mungu tuwekewe amana Injili, ndivyo tunenavyo; si kama wapendezao wanadamu, bali wampendezao Mungu anayetupima mioyo yetu.[#Yer 11:20; Gal 1:10; 1 Tim 1:11]
5Maana hatukuwa na maneno ya kujipendekeza wakati wowote, kama mjuavyo, wala maneno ya juu juu ya kuficha choyo; Mungu ni shahidi.[#Mdo 20:33; Mk 12:40; 2 Pet 2:3]
6Hatukutafuta utukufu kwa wanadamu, wala kwenu, wala kwa wengine, ingawa tungeweza kuwalemea kama Mitume wa Kristo;[#Yn 5:41,44]
7bali tulikuwa wapole katikati yenu, kama vile mlezi awatunzavyo watoto wake mwenyewe.
8Hivyo ndivyo nasi tukiwajali kwa upendo mwingi, tuliona furaha kuwapa, si Injili ya Mungu tu, bali na roho zetu pia, kwa sababu mmekuwa wapendwa wetu.
9Maana, ndugu, mnakumbuka taabu yetu na masumbufu yetu; kwa kuwa mchana na usiku tulifanya kazi tusije tukamlemea mtu wa kwenu awaye yote, huku tukiwahubiria Injili ya Mungu.[#1 Kor 4:12; Mdo 20:34]
10Ninyi ni mashahidi, na Mungu pia, jinsi tulivyokaa kwenu ninyi mnaoamini, kwa utakatifu, na kwa haki, bila kulaumiwa;
11vile vile, kama mjuavyo, jinsi tulivyomwonya kila mmoja wenu kama baba awaonyavyo watoto wake mwenyewe, tukiwatia moyo na kushuhudia;[#Mdo 20:31]
12ili mwende kama ilivyo wajibu wenu kwa Mungu, mwenye kuwaita ninyi ili mwingie katika ufalme wake na utukufu wake.[#Efe 4:1; Flp 1:27; 2 The 1:5; 1 Pet 5:10]
13Kwa sababu hiyo sisi nasi tunamshukuru Mungu bila kukoma, kwa kuwa, mlipopata lile neno la ujumbe wa Mungu mlilolisikia kwetu, mlilipokea si kama neno la wanadamu, bali kama neno la Mungu; na kwa kweli ndivyo lilivyo; litendalo kazi pia ndani yenu ninyi mnaoamini.[#1 The 1:2; Gal 1:11; 2 The 2:13]
14Maana ninyi, ndugu, mlikuwa wafuasi wa makanisa ya Mungu yaliyo katika Yudea, katika Kristo Yesu; kwa kuwa mlipata mateso yale yale kwa watu wa taifa lenu wenyewe, waliyoyapata na hao kwa Wayahudi;[#Mdo 17:5]
15ambao walimwua Bwana Yesu, na hao manabii, na kutuudhi sisi; wala hawampendezi Mungu, wala hawapatani na watu wowote;[#Mdo 2:23; 7:52; 9:23,29; 13:45,50; 14:2,5,19; 17:5,13; 18:12]
16huku wakituzuia tusiseme na Mataifa wapate kuokolewa; ili watimize dhambi zao siku zote. Lakini hasira imewafikia hata mwisho.[#Mwa 15:16; Mt 23:32,33]
17Lakini sisi, ndugu, tukiwa tumefarakana nanyi kwa muda, kwa uso si kwa moyo, tulizidi kutamani kwa shauku nyingi kuwaona nyuso zenu.[#Rum 1:11,13]
18Kwa hiyo tulitaka kuja kwenu, naam, mimi Paulo, nilitaka kuja mara kwa mara, lakini Shetani akatuzuia.
19Maana tumaini letu, au furaha yetu, au taji la kujionea fahari, ni nini? Je! Si ninyi, mbele za Bwana wetu Yesu, wakati wa kuja kwake?[#Flp 2:16; 4:1; 2 The 1:4]
20Maana ninyi ndinyi utukufu wetu, na furaha yetu.