1 Timotheo 1

1 Timotheo 1

Salamu

1Paulo, mtume wa Kristo Yesu, kwa amri ya Mungu Mwokozi wetu na Kristo Yesu, tarajio letu;[#Kol 1:27]

2kwa Timotheo, mwanangu halisi katika imani. Na iwe kwako neema, rehema na amani, zitokazo kwa Mungu Baba na kwa Kristo Yesu Bwana wetu.[#Mdo 16:1; Tit 1:4]

Onyo juu ya waalimu waongo

3Kama vile nilivyokusihi ukae Efeso, nilipokuwa nikisafiri kwenda Makedonia, ili uwakataze wengine wasifundishe elimu nyingine;[#Mdo 20:1]

4wala wasiangalie hadithi na nasaba zisizo na kikomo, zinazozua maswali wala si mpango wa Mungu ulio katika imani; basi uwaambie hivyo.[#1 Tim 4:7; #1:4 ‘Mpango’ katika Kigiriki ni ‘uwakili’.]

5Lakini lengo la agizo hili ni kuleta upendo utokao katika moyo safi na dhamiri njema, na imani isiyo na unafiki.[#Rum 13:10; Gal 5:6]

6Wengine wakiyakosa hayo wamegeukia maneno ya ubatili;[#1 Tim 6:4,20]

7wakitaka kuwa waalimu wa sheria, ingawa hawayafahamu wasemayo wala mambo yale wayanenayo kwa uthabiti.

8Lakini twajua ya kuwa sheria ni njema, kama mtu akiitumia kwa njia iliyo halali;[#Rum 7:12]

9akilifahamu neno hili, ya kuwa sheria haimhusu mtu asiye na hatia, bali wavunjao sheria, waasi, na makafiri, na wenye dhambi, na wanajisi, na wasiomcha Mungu, na wapigao baba zao, na wapigao mama zao, na wauaji,

10na wazinifu, na wafiraji, na waibao watu, na waongo, nao waapao kwa uongo; na linginelo lolote lisilopatana na mafundisho ya kweli;[#1 Tim 6:3]

11kama ilivyonenwa katika Habari Njema ya utukufu wa Mungu ahimidiwaye, niliyowekewa amana.[#1 Tim 6:15]

Shukrani kwa rehema za Mungu

12Nami namshukuru Kristo Yesu Bwana wetu, aliyenitia nguvu kwa sababu aliniona kuwa mwaminifu, akaniweka katika utumishi wake;[#Mdo 9:15; 1 Kor 15:9,10; Gal 1:13-16]

13ingawa hapo awali nilikuwa mtukanaji, mwenye kuudhi watu, mwenye ujeuri, lakini nilipata rehema kwa kuwa nilifanya hivyo kwa ujinga, na kwa kutokuwa na imani.[#Mdo 8:3; 9:4-5]

14Na neema ya Bwana wetu ilizidi sana, pamoja na imani na pendo lililo katika Kristo Yesu.

15Ni neno la kuaminiwa, tena lastahili kukubalika kabisa, ya kwamba Kristo Yesu alikuja ulimwenguni awaokoe wenye dhambi; ambao wa kwanza wao ni mimi.[#Lk 15:2; 19:10]

16Lakini kwa ajili hii nilipata rehema, ili katika mimi wa kwanza, Yesu Kristo audhihirishe uvumilivu wake wote; niwe kielelezo kwa wale watakaomwamini baadaye, wapate uzima wa milele.

17Sasa kwa Mfalme wa milele, asiyeweza kuona uharibifu, asiyeonekana, Mungu peke yake, na iwe heshima na utukufu milele na milele. Amina.[#Rum 16:27]

18Mwanangu Timotheo, nakukabidhi agizo hilo liwe akiba, kwa ajili ya maneno ya unabii yaliyonenwa awali juu yako, ili katika hayo uweze kupigana vile vita vizuri;[#1 Tim 6:12; Yud 1:3]

19uwe mwenye imani na dhamiri njema, ambayo wengine wameisukumia mbali, wakaangamia katika Imani.[#1 Tim 3:9; 6:10]

20Katika hao wamo Himenayo na Iskanda, ambao nimempa Shetani watu hao, ili wafundishwe wasimtukane Mungu.[#2 Tim 2:17; 1 Kor 5:5]

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya