Matendo 1

Matendo 1

Ahadi ya Roho Mtakatifu

1Kitabu kile cha kwanza nilikiandika, Theofilo, kuhusu mambo yote aliyoanza Yesu kufanya na kufundisha,[#Lk 1:1-4]

2hadi siku ile alipochukuliwa juu, alipokuwa amekwisha kuwaagiza kwa Roho Mtakatifu wale mitume aliowachagua;[#Lk 6:13]

3wale aliojidhihirisha kwao kuwa yu hai, kwa dalili nyingi, baada ya kuteswa kwake, akiwatokea muda wa siku arubaini, na kuyanena mambo yaliyouhusu ufalme wa Mungu.

4Wakati alipokuwa amekutana nao aliwaagiza wasitoke Yerusalemu, bali waingoje ahadi ya Baba, ambayo mlisikia habari zake kutoka kwangu;[#Lk 24:49; Mdo 10:41; Yn 15:26]

5ya kwamba Yohana alibatiza kwa maji, bali ninyi mtabatizwa katika Roho Mtakatifu baada ya siku hizi chache.[#Mt 3:11; Mk 1:8; Lk 3:16; Yn 1:33]

Kupaa kwa Yesu

6Basi walipokutanika, wakamwuliza, wakisema, Je! Bwana, wakati huu ndipo unapowarudishia Israeli ufalme?[#Lk 24:21; Mdo 3:21]

7Akawaambia, Si kazi yenu kujua nyakati wala majira, Baba aliyoyaweka katika mamlaka yake mwenyewe.[#Mk 13:32]

8Lakini mtapokea nguvu, akiisha kuwajilia juu yenu Roho Mtakatifu; nanyi mtakuwa mashahidi wangu katika Yerusalemu, na kote katika Yudea, na Samaria, na hata mwisho wa nchi.[#Mt 28:19; Mk 16:15; Lk 24:47-48]

9Akiisha kusema hayo, walipokuwa wakitazama, akainuliwa, wingu likampokea kutoka machoni pao.[#Mk 16:19; Lk 24:50-51; Yn 6:62]

10Walipokuwa wakikaza macho mbinguni, yeye alipokuwa akienda zake, tazama, watu wawili wakasimama karibu nao, wenye nguo nyeupe,[#Lk 24:4]

11wakasema, Enyi watu wa Galilaya, mbona mmesimama mkitazama mbinguni? Huyu Yesu aliyechukuliwa kutoka kwenu kwenda juu mbinguni, atakuja jinsi iyo hiyo mlivyomwona akienda zake mbinguni.[#Mt 26:64; Lk 21:27; 1 Tim 3:16; Ufu 1:7]

Mathiya ateuliwa kuchukua mahali pa Yuda

12Kisha wakarudi kwenda Yerusalemu kutoka mlima ulioitwa wa Mizeituni, ulio karibu na Yerusalemu, wapata mwendo wa sabato.[#Lk 24:50-53]

13Wakati walipoingia, wakapanda ghorofani, walipokuwa wakikaa; Petro, na Yohana, na Yakobo, na Andrea, Filipo na Tomaso, Bartholomayo na Mathayo, Yakobo wa Alfayo, na Simoni Zelote, na Yuda wa Yakobo.[#Mt 10:2-4; Mk 3:16-19; Lk 6:14-16]

14Hawa wote walikuwa wakidumu kwa moyo mmoja katika kusali, pamoja nao wanawake, na Mariamu mama yake Yesu, na ndugu zake.[#Mdo 2:1; Yn 7:3-5; Mt 13:55]

15Siku zile akasimama Petro kati ya hao ndugu (jumla ya majina ilikuwa mia moja na ishirini), akasema,

16Ndugu, ilipasa andiko litimizwe, alilolinena Roho Mtakatifu zamani kwa kinywa cha Daudi, katika habari za Yuda aliyewaongoza wao waliomkamata Yesu;[#Zab 41:9]

17kwa sababu alikuwa amehesabiwa pamoja na sisi, akapata sehemu ya huduma hii.

18(Basi mtu huyu alinunua shamba kwa ijara ya udhalimu; akaanguka kwa kasi akapasuka matumbo yake yote yakatoka.[#Mt 27:3-8]

19Ikajulikana na watu wote wakaao Yerusalemu; hata shamba lile likaitwa kwa lugha yao Akeldama, maana yake, shamba la damu.)

20Kwa maana imeandikwa katika kitabu cha Zaburi,[#Zab 69:25; 109:8]

Kikao chake na kiwe ukiwa,

Wala asiwepo mtu mwenye kukaa humo;

tena,

Usimamizi wake autwae mwingine.

21Basi katika watu waliofuatana nasi wakati wote Bwana Yesu alipokuwa akiingia na kutoka kwetu,[#Yn 15:27]

22kuanza tangu ubatizo wa Yohana, hata siku ile alipochukuliwa kwetu kwenda juu, inapasa mmoja wao awe shahidi wa kufufuka kwake pamoja nasi.[#Mt 3:16; Mk 1:9; 16:19; Lk 3:21; 24:51]

23Wakaweka wawili, Yusufu, aitwaye Barsaba, aliyekuwa na jina la pili Yusto, na Mathiya.

24Kisha wakaomba, wakasema, Wewe, Bwana, ujuaye mioyo ya watu wote, tuoneshe ni nani uliyemchagua katika hawa wawili,[#Yn 2:24,25; 6:70]

25ashike mahali katika huduma hii na utume huu, alioukosa Yuda, aende zake mahali pake mwenyewe.

26Wakawapigia kura; kura ikamwangukia Mathiya; naye akahesabiwa kuwa pamoja na mitume kumi na mmoja.[#Mit 16:33]

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya