Matendo 3

Matendo 3

Petro amponya kiwete mwombaji

1Basi Petro na Yohana walikuwa wakikwea pamoja kwenda hekaluni, saa ya kusali, saa tisa.

2Na mtu mmoja aliyekuwa kiwete toka tumboni mwa mamaye alichukuliwa na watu, ambaye walimweka kila siku katika mlango wa hekalu uitwao Mzuri, ili aombe sadaka kwa watu waingiao ndani ya hekalu.[#Mdo 14:8; Yn 9:1]

3Mtu huyu akiwaona Petro na Yohana wakiingia hekaluni aliomba apewe sadaka.

4Na Petro, akimkazia macho, pamoja na Yohana, akasema, Tutazame sisi.[#Mdo 14:9]

5Akawaangalia, akitaraji kupata kitu kwao.

6Lakini Petro akasema, Mimi sina fedha, wala dhahabu, lakini nilicho nacho ndicho nikupacho. Kwa jina la Yesu Kristo wa Nazareti, simama uende.[#Mdo 3:16]

7Akamshika mkono wa kulia, akamwinua, mara nyayo zake na vifundo vya miguu yake vikatiwa nguvu.

8Akaondoka upesi akasimama, akaanza kwenda; akaingia ndani ya hekalu pamoja nao, akienda, akirukaruka, na kumsifu Mungu.[#Yn 5:14]

9Watu wote wakamwona akienda, akimsifu Mungu.

10Wakamtambua, ya kuwa yeye ndiye aliyekuwa akiketi na kuomba sadaka penye mlango wa hekalu uitwao Mzuri; wakawa na mshangao na kustaajabia mambo yale yaliyompata.

Petro anena katika tao la Sulemani

11Basi alipokuwa akiwashika Petro na Yohana, watu wote wakawakusanyikia mbio katika tao lile lililoitwa tao la Sulemani, wakishangaa sana.[#Mdo 5:12]

12Wakati Petro alipoyaona haya akawajibu wale watu, Enyi Waisraeli, mbona mnastaajabia haya, au mbona mnatukazia macho sisi, kana kwamba tumemfanya huyu aende kwa nguvu zetu sisi, au kwa utauwa wetu sisi?

13Mungu wa Abrahamu na wa Isaka na wa Yakobo, Mungu wa baba zetu, amemtukuza mtumishi wake Yesu, ambaye ninyi mlimsaliti na kumkana mbele ya Pilato, alipokuwa ametoa hukumu yake afunguliwe.[#Kut 3:6,15; Mdo 5:30; Isa 52:13; 53:11; Mdo 2:23]

14Bali ninyi mlimkana yule Mtakatifu, yule Mwenye haki, mkataka mpewe mwuaji;[#Mt 27:15-23; Mk 15:6-14; Lk 23:13-23; Yn 19:12-15]

15mkamwua yule Mkuu wa uzima, ambaye Mungu amemfufua katika wafu; na sisi tu mashahidi wake.[#Mdo 4:10; 5:31; Ebr 2:10]

16Na kwa imani katika jina lake, jina lake limemtia nguvu mtu huyu mnayemwona na kumjua; na imani ile iliyo kwake yeye imempatia huyu uzima huu mkamilifu mbele yenu ninyi nyote.

17Basi sasa, ndugu, najua ya kuwa mliyatenda haya kwa kutokujua kwenu, kama na wakuu wenu walivyotenda.[#Lk 23:34; 1 Tim 1:13]

18Lakini mambo yale aliyohubiri Mungu tangu zamani kwa kinywa cha manabii wake wote, ya kwamba Kristo wake atateswa, ameyatimiza hivyo.[#Lk 24:27]

19Tubuni basi, mrejee, ili dhambi zenu zifutwe, zipate kuja nyakati za kuburudishwa kwa kuwako kwake Bwana;[#Mdo 2:38]

20apate kumtuma Kristo Yesu mliyewekewa tangu zamani;

21ambaye ilimpasa kupokewa mbinguni hata zije zamani za kufanywa upya vitu vyote, zilizonenwa na Mungu kwa kinywa cha manabii wake watakatifu tokea mwanzo wa ulimwengu.

22Kwa maana Musa kweli alisema ya kwamba, Bwana Mungu wenu atawainulieni nabii, katika ndugu zenu, kama mimi; msikieni yeye katika mambo yote atakayonena nanyi.[#Kum 18:15,18; Mdo 7:37]

23Na itakuwa ya kwamba kila mtu asiyemsikiliza nabii huyo ataangamizwa na kutengwa na watu wake.[#Kum 18:19; Law 23:29]

24Naam, na manabii wote tangu Samweli na wale waliokuja baada yake, wote walionena, walihubiri habari za siku hizi.

25Ninyi mmekuwa watoto wa manabii na wa maagano yale, ambayo Mungu aliagana na baba zenu, akimwambia Abrahamu, Katika uzao wako kabila zote za ulimwengu zitabarikiwa.[#Mwa 22:18; 12:3; Gal 3:8]

26Mungu, akiisha kumfufua mtumishi wake Yesu, alimtuma kwenu ninyi kwanza, ili kuwabariki kwa kumwepusha kila mmoja wenu na maovu yake.[#Mdo 13:46]

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya