Kutoka 23

Kutoka 23

Haki kwa wote

1Usivumishe habari za uongo; usishirikiane na mwovu kwa kuwa shahidi wa uongo.[#Kut 20:16; Law 19:11-12; Kum 5:20; Mit 10:18; 1 Fal 21:10; Mit 19:5; Mdo 6:11]

2Usiwafuate walio wengi kutenda uovu; wala usitie ushahidi wako katika neno lolote kwa kugeukia kando na kuandamana na mkutano ili kupotoa hukumu;[#1 Fal 19:10; Ayu 31:34; Lk 23:23; Zab 72:2]

3wala usimpendelee mtu mnyonge katika neno lake.[#Law 19:15]

4Ukimwona ng'ombe wa adui wako, au punda wake, amepotea, sharti umrudishie mwenyewe tena.[#Kum 22:1-4; Mit 25:21; 1 The 5:15]

5Ukimwona punda wake huyo akuchukiaye akiwa ameanguka chini ya mzigo wake, na wewe ungejizuia usimsaidie, lazima umsaidie.

6Usipotoe hukumu ya mtu maskini katika neno lake.[#Law 19:15; Kum 16:19; Ayu 31:13]

7Jitenge mbali na neno la uongo; wala wasio hatia na wenye haki usiwaue; kwa kuwa mimi sitamhesabia haki yeye aliye mwovu.[#Efe 4:25; Rum 1:18]

8Nawe usipokee rushwa; kwani hiyo rushwa huwapofusha macho hao waonao, na kuyapotoa maneno ya wenye haki.[#Mit 17:8]

9Usimwonee mgeni; maana, ninyi mwajua moyo wa mgeni ulivyo, kwa kuwa ninyi mlikuwa wageni katika nchi ya Misri.[#Zab 94:6; Kut 22:21; Law 19:33-34; Kum 24:17-18; 27:19]

Sheria kuhusu mwaka wa saba na Sabato

10Utapanda mbegu katika nchi yako muda wa miaka sita na kupata mavuno yake;[#Law 25:1-7]

11lakini mwaka wa saba utaiacha nchi ipumzike na kutulia; hao maskini miongoni mwa watu wako wapate kula; na hicho watakachosaza wao, wapate kula wanyama wa kondeni. Utafanya vivyo hivyo katika shamba lako la mizabibu, na katika shamba lako la mizeituni.

12Siku sita utafanya kazi yako, na siku ya saba utapumzika; ili kwamba ng'ombe wako na punda wako wapate kupumzika, kisha mwana wa mjakazi wako na mgeni wapate kuburudika.[#Lk 13:14; Kut 20:9-11; 31:15; 34:21; 35:2; Law 23:3; Kum 5:13-14]

13Yaangalieni hayo yote niliyowaambia; wala msitaje kabisa majina ya miungu mingine, wala yasisikizwe kutoka kinywani mwako.[#Hos 2:17]

Sikukuu za kila mwaka

14Mara tatu kila mwaka utaniwekea sikukuu.[#Kum 16:16]

15Utaiweka sikukuu ya mikate isiyotiwa chachu; utakula mikate isiyochachwa muda wa siku saba kama nilivyokuagiza, kwa wakati uliowekwa, mwezi wa Abibu (kwa maana ndio mwezi uliotoka Misri); wala hapana mtu atakayeonekana mbele yangu na mikono mitupu;[#Kut 12:14-20; Law 23:6-8; Hes 28:17-25]

16tena, sikukuu ya mavuno, hayo malimbuko ya kazi zako za kupanda mashambani; tena, sikukuu ya kukusanya, mwisho wa mwaka, hapo utakapokusanya hayo uliyoyataabikia shambani.[#Law 23:15-21,39-43; Hes 28:26-31; #23:16 Kwingineko ni sikukuu ya vibanda.]

17Mara tatu katika mwaka wana wa kiume wako wote watahudhuria mbele ya Bwana MUNGU.

18Usinitolee damu ya dhabihu zangu pamoja na mkate uliotiwa chachu, wala mafuta ya sikukuu yangu usiyaache kusalia hadi asubuhi.

19Ya kwanza ya malimbuko ya nchi yako utayaleta na kuyatia ndani ya nyumba ya BWANA, Mungu wako. Usimtokose mwana-mbuzi katika maziwa ya mama yake.[#Kut 34:26; Kum 14:21; 26:2; Neh 10:35; Mit 3:9]

Kuahidiwa Ushindi juu ya Kanaani

20Tazama, mimi namtuma malaika aende mbele yako, ili akulinde njiani na kukupeleka mpaka mahali pale nilipokuandalia.

21Jitunzeni mbele yake, muisikize sauti yake; wala msimtie kasirani; maana, hatawasamehe makosa yenu; kwa kuwa jina langu limo ndani yake.[#Efe 4:30; Yos 24:19; 1 Yoh 5:16; Isa 9:6; Yer 23:6; Yn 10:38]

22Lakini ukiisikiza sauti yake kweli, na kuyatenda yote ninenayo mimi; ndipo mimi nitakuwa ni adui wa adui zako, na mtesi wa hao wakutesao.[#Mwa 12:3]

23Kwa kuwa malaika wangu atatangulia mbele yako, na kukufikisha kwa Mwamori, na Mhiti, na Mperizi, na Mkanaani, na Mhivi, na Myebusi; nami nitawatupilia mbali.[#Yos 24:8]

24Usiisujudie miungu yao, wala kuitumikia; wala usitende mfano wa matendo yao; bali utaiangamiza kabisa, na nguzo zao utazivunja vipande vipande.[#Kut 20:5]

25Nanyi mtamtumikia BWANA, Mungu wenu, naye atakibarikia chakula chako, na maji yako; nami nitakuondolea ugonjwa kati yako.[#Kum 10:12; Yos 22:5; 1 Sam 2:20; Mt 4:10; Kum 7:15; 28:5]

26Hapatakuwa na mwenye kuharibu mimba, wala aliye tasa, katika nchi yako; na hesabu ya siku zako nitaitimiza.[#Ayu 21:10; Mwa 25:8]

27Nitatuma utisho wangu utangulie mbele yako, nami nitawafadhaisha watu wote utakaowafikia, nami nitawafanya hao adui zako wote wakuoneshe maungo yao.[#Mwa 35:5; Kum 2:25; Yos 2:9,11; 1 Sam 14:15]

28Nami nitapeleka mavu mbele yako, watakaomfukuza Mhivi, na Mkanaani, na Mhiti, watoke mbele yako.[#Kum 7:20; #23:28 Maana si dhahiri neno hili lina maana ya ‘dondora’, maradhi mabaya au ‘baa’.]

29Sitawafukuza mbele yako katika mwaka mmoja; nchi isiwe ukiwa, na wanyama wa pori wakaongezeka na kukusumbua.[#Kum 7:22]

30Nitawafukuza kidogo kidogo mbele yako, hata utakapoongezeka wewe, na kuirithi hiyo nchi.

31Nami nitakuwekea mpaka wako tangu Bahari ya Shamu hadi bahari ya Wafilisti, tena tangu jangwani hata huo Mto; kwa kuwa nitawatia wenyeji wa nchi mkononi mwako; nawe utawafukuza mbele yako.[#1 Fal 4:21; Yos 21:44]

32Usifanye maagano pamoja nao, wala pamoja na miungu yao.

33Wasikae katika nchi yako, wasije wakakufanya kunitendea mimi dhambi; kwa sababu ukiitumikia miungu yao, jambo hili halikosi litakuwa ni (mtego) tanzi kwako.[#Kut 34:12,15; Kum 7:2; 12:30; Yos 23:13; Amu 2:3; 1 Sam 18:21; Zab 106:36,37]

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya