Kutoka 30

Kutoka 30

Madhabahu ya kufukizia uvumba

1Nawe fanya madhabahu ya kufukizia uvumba; utaifanyiza kwa mti wa mshita.[#Kut 37:25; 40:5; Ufu 8:3]

2Urefu wake utakuwa dhiraa moja, na upana wake dhiraa moja; itakuwa mraba; na kwenda juu kwake dhiraa mbili; pembe zake zitakuwa za kitu kimoja nayo.

3Nawe utaifunikiza dhahabu safi juu yake, na mbavu zake kandokando, na pembe zake; nawe utaifanyia ukingo wa dhahabu kuizunguka.

4Kisha utaifanyia pete mbili za dhahabu, chini ya ukingo wake katika mbavu zake mbili, katika pande zake mbili utazifanya; nazo zitakuwa mahali pa kuitia miti ya kuichukulia.

5Na ile miti utaifanya kwa mti wa mshita, na kuifunikiza dhahabu safi.

6Nawe utaitia mbele ya lile pazia lililo karibu na sanduku la ushuhuda mbele ya kiti cha rehema kilicho juu ya ushuhuda, hapo nitakapokutana nawe.

7Na Haruni atafukiza uvumba wa manukato juu yake; kila siku asubuhi atakapozitengeneza zile taa, ataufukiza.

8Na Haruni atakapoziwasha zile taa wakati wa jioni, ataufukiza, uwe uvumba wa daima mbele za Bwana katika vizazi vyenu vyote.

9Hamtafukiza juu yake uvumba mgeni, wala sadaka ya kuteketezwa, wala sadaka ya unga, wala hamtamimina juu yake sadaka ya kinywaji.[#Law 10:1]

10Naye Haruni atafanya upatanisho juu ya pembe zake mara moja kila mwaka; kwa damu ya ile sadaka ya dhambi ya kufanya upatanisho, mara moja kila mwaka ataifanyia upatanisho, katika vizazi vyenu vyote; ni takatifu sana kwa BWANA.[#Law 23:27]

Nusu shekeli ya mahali patakatifu

11BWANA akanena na Musa, na kumwambia,

12Utakapowahesabu wana wa Israeli, kama itakavyotokea hesabu yao, ndipo watakapompa BWANA kila mtu ukombozi kwa ajili ya roho yake, hapo utakapowahesabu; ili kwamba yasiwe maradhi kati yao, hapo utakapowahesabu.[#Kut 38:25; Hes 1:2,5; 26:2; 2 Sam 24:2; Ayu 33:24; 36:18; Zab 49:7; Mt 20:28; Mk 10:45; 1 Tim 2:6; 1 Pet 1:18; 2 Sam 24:15]

13Nacho watakachotoa ni hiki, kila mtu apitaye kwa wale waliohesabiwa atatoa nusu shekeli kwa kuiandama shekeli ya mahali patakatifu; (shekeli ni gera ishirini;) nusu shekeli kwa sadaka ya BWANA.[#Kut 38:25-26; Mt 17:24; Hes 3:47; Eze 45:12]

14Kila mtu apitaye kwa wale waliohesabiwa tangu huyo ambaye umri wake ni miaka ishirini, au zaidi, atatoa hiyo sadaka ya BWANA.

15Matajiri hawataleta zaidi, wala maskini hawataleta kilichopungua, katika hiyo nusu shekeli, watakapotoa hiyo sadaka ya BWANA, ili kufanya upatanisho kwa ajili ya roho zenu.[#Ayu 34:19; Mit 22:2; Mdo 10:34; Rum 2:11; Gal 2:6; Efe 6:9; Kol 3:25; 1 Pet 1:17]

Birika la shaba

16Nawe utapokea hizo fedha za upatanisho mikononi mwa hao wana wa Israeli, na kuziweka kwa ajili ya utumishi wa hema ya kukutania; ili kwamba ziwe ukumbusho kwa ajili ya wana wa Israeli mbele ya BWANA, ili kufanya upatanisho kwa ajili ya roho zenu.[#Hes 16:40]

17BWANA akanena na Musa, na kumwambia

18Fanya na birika la shaba, na kitako chake cha shaba, ili kuogea; nawe utaliweka kati ya hema ya kukutania na madhabahu, nawe utalitia maji.[#Kut 38:8; 1 Fal 7:38]

19Na Haruni na wanawe wataosha mikono yao na miguu yao humo;[#Isa 52:11; Ebr 10:22]

20hapo waingiapo ndani ya hema ya kukutania; watajiosha majini, ili wasife; au hapo watakapoikaribia madhabahu ili watumike, kumteketezea BWANA sadaka ya moto;

21basi wataosha mikono yao na miguu yao ili kwamba wasife; na neno hili litakuwa amri kwao milele, kwake yeye na kwa wazao wake katika vizazi vyao vyote.[#Kut 28:43]

Kupaka mafuta na uvumba wa manukato

22Kisha BWANA akasema na Musa, na kumwambia,[#Kut 37:29]

23Jitwalie manukato yaliyo bora, manemane mbichi shekeli mia tano, na mdalasini wenye harufu nzuri nusu ya kiasi hicho, yaani, shekeli mia mbili na hamsini, na miwa shekeli mia mbili na hamsini,[#Wim 4:14; Eze 27:22; Zab 45:8; Yer 6:20]

24na kida shekeli mia tano, kwa kuiandama shekeli ya mahali patakatifu, na mafuta ya zeituni kiasi cha vibaba vitano;[#Zab 45:8; Kut 29:40]

25nawe utayafanya mafuta ya kutiwa matakatifu, marhamu iliyochanganywa kwa kazi ya ustadi ya mtengezaji manukato; yatakuwa ni mafuta matakatifu ya kutiwa.[#Hes 35:25; Zab 89:20; 133:2]

26Nawe utaipaka hema ya kukutania kwa mafuta hayo, na hilo sanduku la ushuhuda,[#Law 8:10; Hes 7:1]

27na hiyo meza, vyombo vyake vyote, kinara cha taa, vyombo vyake na madhabahu ya kufukizia uvumba,

28na madhabahu ya kuteketezea sadaka, pamoja na vyombo vyake vyote, na birika, na kitako chake.

29Nawe utavitakasa vitu hivyo, ili viwe vitakatifu sana; tena kila kivigusacho vyombo vile kitakuwa kitakatifu.

30Nawe utawatia mafuta Haruni na wanawe, kuwaweka wakfu, ili wanitumikie wakiwa makuhani.

31Nawe utanena na wana wa Israeli na kuwaambia, Haya yatakuwa ni mafuta matakatifu ya kutiwa kwa ajili yangu mimi katika vizazi vyenu vyote.

32Hayatamiminwa katika kiwiliwili cha binadamu, wala msifanye mengine mfano wa haya kama yalivyoungwa kwa viungo vyake; ni matakatifu, na kwenu ninyi yatakuwa matakatifu.

33Mtu yeyote atakayechanganya mafuta mfano wa haya, au mtu yeyote atakayetia mafuta haya juu ya mgeni, mtu huyo atatengwa mbali na watu wake.[#Mwa 17:14; Law 7:20,21]

34BWANA akamwambia Musa, Jitwalie manukato mazuri, yaani, natafi, na shekelethi, na kelbena; viungo vya manukato vizuri pamoja na ubani safi; vitu hivyo vyote na viwe vya kipimo kimoja;[#Kut 25:6; 37:29]

35nawe utafanya uvumba wa vitu hivyo, manukato ya kazi ya ustadi wa mtengenezaji manukato, yatakuwa yamekolea, safi, matakatifu;

36nawe baadhi yake utayaponda sana, na kuyaweka mbele ya ushuhuda ndani ya hema ya kukutania, hapo nitakapokutana nawe; nayo yatakuwa kwenu matakatifu sana.[#Kut 29:37,42; Law 2:3; 16:2]

37Na uvumba utakaofanya, hamtajifanyia uvumba wenye viungo sawasawa na uvumba huo; utakuwa kwenu mtakatifu kwa ajili ya BWANA.

38Mtu yeyote atakayefanya mfano wa huo, ili kuunusa, mtu huyo atatengwa mbali na watu wake.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya