Kutoka 31

Kutoka 31

Bezaleli na Oholiabu

1BWANA akanena na Musa, na kumwambia,

2Angalia, nimemwita kwa jina lake Bezaleli mwana wa Uri, mwana wa Huri, wa kabila la Yuda;[#Kut 35:30; 1 Nya 2:20]

3nami nimemjaza Roho ya Mungu, katika hekima, na maarifa, na ujuzi, na mambo ya kazi ya kila aina,[#Kut 35:31; 1 Fal 7:14; Isa 28:26; 1 Kor 12:4-8]

4ili abuni kazi za ustadi, kuwa fundi wa dhahabu, na wa fedha, na wa shaba,

5na kukata vito kwa kutiwa mahali, na kuchora miti, na kufanya kazi ya ustadi iwayo yote.

6Tena, tazama, nimemchagua, awe pamoja naye, huyo Oholiabu, mwana wa Ahisamaki, wa kabila la Dani; nami nimetia hekima katika mioyo ya wote wenye moyo wa hekima, ili wapate kutengeneza vyote nilivyokuagiza;[#Kut 35:34; 28:3; 36:1]

7yaani, hema ya kukutania na sanduku la ushuhuda, na kiti cha rehema kilicho juu yake, na vyombo vyote vya Hema;[#Kut 36:8]

8na meza, na vyombo vyake, na kinara cha taa safi pamoja na vyombo vyake vyote, na madhabahu ya kufukizia uvumba;

9na madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa na vyombo vyake vyote, na birika na kitako chake;

10na mavazi yenye kufumwa kwa uzuri, na mavazi matakatifu ya Haruni kuhani, na mavazi ya wanawe, ili kutumika kwa ajili ya huduma yao ya ukuhani;

11na mafuta ya kutiwa, na uvumba wa manukato mazuri, kwa ajili ya mahali patakatifu; sawasawa na yote niliyokuagiza ndivyo watakavyofanya wao.

Sheria za Sabato

12BWANA akasema na Musa, na kumwambia,

13Kisha, nena na wana wa Israeli, na kuwaambia, Hakika mtazishika Sabato zangu, kwa kuwa ni ishara kati yenu na mimi katika vizazi vyenu vyote; ili mpate kujua ya kuwa mimi ndimi BWANA niwatakasaye ninyi.[#Law 19:3; 26:2; Eze 20:12; 44:24]

14Basi mtaishika hiyo Sabato; kwa kuwa ni takatifu kwenu; kila mtu atakayeitia unajisi hana budi atauawa; na kila mtu afanyaye kazi siku hiyo, ataondolewa toka kwa watu wake.[#Neh 9:14; Kum 5:12; Isa 56:6; 58:13; Eze 20:12; Kut 35:2; Hes 15:35]

15Kazi itafanywa siku sita; lakini siku ya saba ni Sabato ya kustarehe kabisa, takatifu kwa BWANA; kila mtu atakayefanya kazi yoyote katika siku ya Sabato, hana budi atauawa.[#Mwa 2:2; Kut 16:23; 20:8-11; 23:12; 28:36; 34:21; 35:2; Law 23:3; Kum 5:12-14]

16Kwa ajili ya hayo wana wa Israeli wataishika Sabato, kuiangalia sana hiyo Sabato katika vizazi vyao vyote, ni agano la milele.

17Ni ishara kati ya mimi na wana wa Israeli milele; kwani kwa siku sita BWANA alifanya mbingu na nchi, akapumzika kwa siku ya saba na kustarehe.[#Kut 20:11; Eze 20:12; Mwa 1:31]

Mbao mbili za mawe ni ushuhuda wa Agano

18Hapo BWANA alipokuwa amekwisha zungumza na Musa katika mlima wa Sinai, akampa hizo mbao mbili za ushuhuda, mbao mbili za mawe, zilizoandikwa kwa kidole cha Mungu.[#Kut 24:12; 32:15; 34:28,29; Kum 4:13; 5:22; 9:10,11; 2 Kor 3:3; #31:18 Katika Kiebrania hakuna neno BWANA ila hutaja nafsi ya tatu umoja jaani: ‘alipokuwa’.]

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya