Hosea 10

Hosea 10

Dhambi ya Israeli na kutekwa kwake

1Israeli ni mzabibu mzuri, utoao matunda yake; kwa kadiri ya wingi wa matunda yake, kwa kadiri iyo hiyo ameongeza madhabahu zake; kwa kadiri ya wema wa nchi yake, kwa kadiri iyo hiyo wamefanya nguzo nzuri.

2Moyo wao umegawanyika; sasa wataonekana kuwa na hatia; yeye atazipiga madhabahu zao, ataziharibu nguzo zao.

3Yakini sasa watasema, Hatuna mfalme; kwa maana hatumchi BWANA; na mfalme huyu je! Aweza kututendea nini?

4Hunena maneno yasiyo na maana; huapa kwa uongo wafanyapo maagano; basi ndipo hukumu huchipuka kama mbaruti katika matuta ya shamba.

5Wakaao Samaria wataona hofu kwa ajili ya ndama za Beth-aveni; kwa maana watu wa mji huo wataulilia, na makuhani wake walioufurahia, kwa sababu ya utukufu wake; kwa maana umetoweka.[#1 Fal 12:28; 2 Fal 10:29; 2 Nya 11:15; Hos 8:5,6]

6Nayo itachukuliwa Ashuru, iwe zawadi kwa mfalme Yarebu; Efraimu atapata aibu, na Israeli atalionea haya shauri lake mwenyewe.[#Hos 5:13]

7Katika habari za Samaria, mfalme wake amekatiliwa mbali, kama povu usoni pa maji.

8Mahali pa Aveni palipoinuka, yaani, dhambi ya Israeli, pataharibika; mwiba na mbigili itamea juu ya madhabahu zake; nao wataiambia milima, Tusitirini; na vilima, Tuangukieni.[#Kum 9:21; Lk 23:30; Ufu 6:16]

9Ee Israeli, umefanya dhambi tangu siku za Gibea; huko ndiko walikosimama; Je, vita juu ya wana wa uovu hakitawapata katika Gibea?[#Amu 19:1-30]

10Wakati nitakapopenda nitawaadhibu; na hao mataifa watakusanyika juu yao, watakapofungwa kwa sababu ya makosa yao mawili.[#Kum 28:63; 1 Fal 14:16; Amo 8:14]

11Naye Efraimu ni ndama aliyefundishwa, apendaye kupura; lakini nimepitisha kongwa juu ya shingo yake nzuri; nitampandisha mwenye kupanda juu ya Efraimu; Yuda atalima, na Yakobo atapiga haro yeye mwenyewe.

12Jipandieni katika haki, vuneni kwa fadhili; uchimbueni udongo wa mashamba yenu, kwa maana wakati umewadia wa kumtafuta BWANA, hata atakapokuja na kuwanyeshea haki.[#Mit 11:18; Mhu 11:6; Isa 32:20; Yak 3:18; Yer 4:3]

13Mmelima dhuluma, mmevuna uovu; mmekula matunda ya uongo; kwa maana uliitumainia njia yako, na wingi wa mashujaa wako.[#Ayu 4:8; Mit 22:8; Hos 8:7]

14Kwa sababu hiyo fitina itatokea kati ya watu wako, na ngome zako zote zitaharibiwa, kama vile Shalmani alivyoharibu Betharbeli, katika siku ya vita; mama akavunjikavunjika pamoja na watoto wake.[#2 Fal 18:34]

15Hivyo ndivyo Betheli atakavyowatenda ninyi, kwa sababu ya ubaya wenu mwingi; wakati wa mapambazuko mfalme wa Israeli atakatiliwa mbali kabisa.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya