The chat will start when you send the first message.
1Basi neno la BWANA lilimjia Yona, mwana wa Amitai, kusema,[#2 Fal 14:25]
2Ondoka, uende Ninawi, mji ule mkubwa, ukapige kelele juu yake; kwa maana uovu wao umepanda juu mbele zangu.[#Mwa 10:11; 18:20; Yon 3:3; Nah 2:8; Mt 12:41; Ezr 9:6; Yak 5:4]
3Lakini Yona akaondoka akimbilie Tarshishi, apate kujiepusha na uso wa BWANA; akateremka hadi Yafa, akaona merikebu inayokwenda Tarshishi; basi, akalipa nauli, akapanda merikebuni, aende pamoja nao Tarshishi, ajiepushe na uso wa BWANA.[#Isa 23:1; Yos 19:46; 2 Nya 2:16; Mdo 9:36; Mwa 4:16]
4Lakini BWANA alituma upepo mkuu baharini, ikawa tufani kubwa baharini, hata merikebu ikawa karibu kuvunjika.
5Basi wale mabaharia wakaogopa, kila mtu akamwomba mungu wake; nao wakatupa baharini shehena iliyokuwa merikebuni, ili kuupunguza uzito wake. Lakini Yona alikuwa ameshuka hadi pande za ndani za merikebu; akajilaza, akapata usingizi.
6Basi nahodha akamwendea, akamwambia, Una nini, Ewe ulalaye usingizi? Amka, ukamwombe Mungu wako; labda Mungu huyo atatukumbuka, tusipotee.[#Zab 78:34; Mt 8:25]
7Wakasemezana kila mtu na mwenzake, Haya, na tupige kura, tupate kujua mabaya haya yametupata kwa sababu ya nani. Basi wakapiga kura, nayo kura ikamwangukia Yona.[#Yos 7:14; 1 Sam 10:20; Mit 16:33; Mdo 1:26]
8Ndipo wakamwambia, Tafadhali utuambie, wewe ambaye mabaya haya yametupata kwa sababu yako; kazi yako ni kazi gani? Nawe umetoka wapi? Nchi yako ni nchi ipi? Nawe u mtu wa kabila gani?[#Yos 7:19]
9Akawaambia, Mimi ni Mwebrania; nami namcha BWANA, Mungu wa mbingu, aliyeziumba bahari na nchi kavu.
10Ndipo watu wale wakaogopa mno, wakamwambia, Ni jambo gani hili ulilolitenda! Kwa maana watu wale walijua ya kuwa amekimbia, ajiepushe na uso wa BWANA, kwa sababu alikuwa amewaambia.
11Basi wakamwambia, Tukutende nini, ili bahari itulie? Kwa maana bahari ilikuwa inazidi kuchafuka.
12Naye akawaambia, Nikamateni, mnitupe baharini; kisha bahari itatulia; kwa maana najua ya kuwa ni kwa ajili yangu tufani hii imewapata.[#Mhu 9:18]
13Lakini wale watu wakavuta makasia kwa nguvu, ili wapate kurudi pwani, wasiweze; kwa maana bahari ilizidi kuwachafukia sana.[#Mit 21:30]
14Basi wakamlilia BWANA, wakasema, Twakuomba, Ee BWANA, twakuomba, tusiangamie kwa ajili ya uhai wa mtu huyu, wala usitupatilize kwa ajili ya damu isiyo na hatia; kwa maana wewe, BWANA, umefanya kama ulivyopenda.[#Kum 21:8]
15Basi wakamkamata Yona, wakamtupa baharini, nayo bahari ikaacha kuchafuka.
16Ndipo wale watu wakamwogopa BWANA mno, wakamtolea BWANA sadaka, na kuweka nadhiri.
17BWANA akaweka tayari samaki mkubwa ili ammeze Yona, naye Yona akawa ndani ya tumbo la samaki yule muda wa siku tatu, mchana na usiku.[#Mt 12:40]