The chat will start when you send the first message.
1Kisha BWANA akanena na Musa, na kumwambia,
2Nena na Haruni na wanawe, ili washughulikie kwa uangalifu vitu vitakatifu vya wana wa Israeli ambavyo wanitakasia mimi, tena wasilinajisi jina langu takatifu; mimi ndimi BWANA.[#Hes 6:3; 15:31; Kut 13:12; 28:38; Hes 18:32; Kum 15:19]
3Waambie, Mtu yeyote wa kizazi chenu chote katika vizazi vyenu, atakayevikaribia vile vitu vitakatifu, ambavyo wana wa Israeli wamtakasia BWANA, naye ana unajisi, mtu huyo atatengwa asiwe mbele zangu; mimi ndimi BWANA.[#Law 7:20]
4Mtu yeyote wa kizazi cha Haruni aliye na ukoma, au kisonono; asile katika vitu vitakatifu, hata atakapokuwa safi. Tena mtu yeyote atakayekinusa kitu kilicho na unajisi kwa sababu ya wafu, au mtu ambaye shahawa humtoka;[#Law 15:2,13; Hes 19:11,22]
5au mtu amgusaye mnyama atambaaye, wa kumpatia unajisi, au kwamba amgusa mtu wa kumpatia unajisi, kwa unajisi wowote ule alio nao;[#Law 11:24; 15:7,19]
6huyo mtu atakayegusa kitu chochote namna hiyo atakuwa najisi hata jioni, naye hatakula katika vitu vitakatifu, asipooga mwili wake majini.[#Ebr 10:22]
7Jua likiisha kuchwa atakuwa safi; kisha baadaye atakula katika vitu vitakatifu, maana ni chakula chake.[#Hes 18:11]
8Nyamafu au mnyama aliyeraruliwa na wanyama asile, asijitie unajisi kwa hiyo nyama; mimi ndimi BWANA.[#Kut 22:31; Law 17:15; Eze 44:31]
9Basi kwa hiyo watayashika maagizo yangu, wasije wakachukua dhambi kwa hayo, nao wakafa humo, wakiyanajisi; mimi ndimi BWANA niwatakasaye.[#Kut 28:43; Hes 18:22]
10Mgeni yeyote asile katika kitu kitakatifu; mgeni wa kuhani akaaye kwake, au mtumishi aliyeajiriwa, asile katika kitu kitakatifu.[#Kut 29:33; Hes 3:10; 1 Sam 21:6]
11Lakini kuhani akinunua mtu yeyote kwa fedha zake, yeye atakula katika hicho; na hao waliozaliwa nyumbani mwake watakula katika chakula chake.
12Na binti ya kuhani ikiwa ameolewa na mgeni, asile katika sadaka ya kuinuliwa katika vitu vile vitakatifu.
13Lakini ikiwa binti ya kuhani ni mjane, au ameachwa na mumewe, wala hana mtoto, kisha amerudi na kuishi katika nyumba ya baba yake, kama vile katika ujana wake, yeye atakula katika chakula cha baba yake; lakini mgeni yeyote asile katika chakula hicho.[#Mwa 38:11; Hes 18:11]
14Tena kama mtu yeyote akila katika kitu kilicho kitakatifu pasipo kukijua, ndipo ataongeza sehemu ya tano juu ya kitu hicho, na kumpa kuhani kitu hicho kitakatifu.[#Law 5:15,16]
15Wala wasivinajisi vitu vitakatifu vya wana wa Israeli, wavisongezavyo kwa BWANA;[#Hes 18:32]
16hata wakawatwika ule uovu uletao hatia, hapo walapo vitu vyao vitakatifu; kwa kuwa mimi ndimi BWANA niwatakasaye.
17Kisha BWANA akanena na Musa, na kumwambia,
18Nena na Haruni na wanawe, na wana wa Israeli wote, uwaambie, Mtu yeyote wa nyumba ya Israeli, au wa wageni walio katika Israeli, atakayetoa matoleo yake, kama ni mojawapo ya nadhiri zao, au kama ni sadaka yoyote ya hiari, watakayomtolea BWANA kuwa sadaka ya kuteketezwa;[#Hes 15:14]
19ili mpate kukubaliwa, mtaleta dume mkamilifu, katika ng'ombe, au katika kondoo, au katika mbuzi.
20Lakini mnyama yeyote aliye na kilema msimtoe; kwa kuwa hatakubaliwa kwa ajili yenu.[#Kum 17:1; 15:21; Mal 1:8,14; Efe 5:27; Ebr 9:14; 1 Pet 1:19]
21Na mtu yeyote atakayemtolea BWANA dhabihu katika sadaka za amani, ili kuondoa nadhiri, au sadaka ya moyo wa kupenda, katika ng'ombe, au katika kondoo, atakuwa mkamilifu, apate kukubaliwa; pasiwe na kilema chochote ndani yake.[#Hes 15:3,8; Kum 23:21; Zab 61:8; 65:1; Mhu 5:4,5]
22Kipofu, au aliyevunjika mahali, au kiwete au aliye na vidonda, au aliye na upele, au aliye na upele, hamtamtolea BWANA wanyama hao, wala msiwasongeze kwa BWANA kwa njia ya moto juu ya madhabahu.
23Ng'ombe, au mwana-kondoo aliye na kitu kilichozidi, au aliyepungukiwa na kitu katika vitu vya mwilini mwake, mna ruhusa kutoa kuwa sadaka ya moyo wa kupenda; lakini kwa ajili ya nadhiri hatakubaliwa.[#Law 21:18]
24Mnyama aliyeumia mapumbu yake, au kusetwa, au kuvunjwa, au kukatwa, msimtolee BWANA; wala msifanye hivi katika nchi yenu.
25Wala msisongeze chakula cha Mungu wenu katika wanyama hao mmojawapo kitokacho mkononi mwa mgeni; kwa sababu uharibifu wao uko ndani yao, wana kilema ndani yao; hawatakubaliwa kwa ajili yenu.[#Hes 15:15; Mal 1:14]
26Kisha BWANA akanena na Musa, na kumwambia,
27Hapo ng'ombe, kondoo au mbuzi, akizaliwa, atakuwa pamoja na mamaye muda wa siku saba; na siku ya nane na baadaye atakubaliwa kuwa ni sadaka ya kutolewa kwa BWANA kwa njia ya moto.[#Kut 22:30]
28Tena kama ni ng'ombe, au kondoo, msimchinje huyo na mwanawe, wote wawili kwa siku moja.[#Kum 22:6]
29Tena mtakapomchinjia BWANA dhabihu ya shukrani, mtamchinja ili mpate kukubaliwa.[#Zab 107:22; 116:17; Amo 4:5]
30Italiwa siku iyo hiyo; msisaze kitu chake hata asubuhi; mimi ndimi BWANA.
31Kwa hiyo mtayashika maagizo yangu, na kuyafanya; mimi ndimi BWANA.[#Law 19:37; Hes 15:40; Kum 4:40]
32Wala msilinajisi jina langu takatifu; lakini nitatakaswa mimi katika wana wa Israeli; mimi ndimi BWANA niwatakasaye ninyi,[#Isa 6:3; Mt 6:9; Lk 11:2; Yn 12:28]
33niliyewaleta mtoke nchi ya Misri, ili niwe Mungu wenu; mimi ndimi BWANA.[#Kut 6:7]