Luka 24

Luka 24

Kufufuka kwa Yesu

1Siku ya kwanza ya juma, ilipoanza kupambazuka, walikwenda kaburini, wakiyaleta manukato waliyoweka tayari.[#Mt 28:1-8; Mk 16:1-8; Yn 20:1-13]

2Wakalikuta lile jiwe limevingirishwa mbali na kaburi,

3Wakaingia, wasiuone mwili wa Bwana Yesu.

4Ikawa walipokuwa wakifadhaika kwa ajili ya neno hilo, tazama, watu wawili walisimama karibu nao, wamevaa nguo za kumetameta;

5nao walipoingiwa na hofu na kuinama kifudifudi hadi nchini, hao waliwaambia, Kwa nini mnamtafuta aliye hai katika wafu?

6Hayupo hapa, amefufuka. Kumbukeni alivyosema nanyi alipokuwa bado yuko Galilaya,[#Mt 16:21; 17:22-23; 20:18-19; Mk 8:31; 9:31; 10:33-34; Lk 9:22; 18:31-33]

7akisema, Imempasa Mwana wa Adamu kutiwa mikononi mwa wenye dhambi, na kusulubiwa, na kufufuka siku ya tatu.

8Wakayakumbuka maneno yake.

9Wakaondoka kaburini, wakarudi; wakawaarifu wale kumi na mmoja na wengine wote habari za mambo hayo yote.

10Nao ni Mariamu Magdalene, na Yoana, na Mariamu mamaye Yakobo, na wale wanawake wengine waliokuwa pamoja nao;[#Lk 8:2,3]

11hao waliwaambia mitume habari ya mambo hayo.

12Maneno yao yakaonekana kuwa kama upuzi kwao, wala hawakuwasadiki. Lakini Petro aliondoka akaenda mbio hadi kaburini, akainama akachungulia ndani, akaviona vile vitambaa vya sanda tu; akaenda zake akiyastaajabia yaliyotukia.

Matembezi ya kwenda Emau

13Na tazama, siku ile ile watu wawili miongoni mwao walikuwa wakienda katika kijiji kimoja, jina lake Emau, kilichokuwa mbali na Yerusalemu kama mwendo wa saa mbili.[#Mk 16:12,13]

14Nao walikuwa wakizungumza wao kwa wao habari za mambo hayo yote yaliyotukia.

15Ikawa katika kuzungumza na kuulizana kwao, Yesu mwenyewe alikaribia, akaandamana nao.[#Mt 18:20]

16Macho yao yakafumbwa wasimtambue.

17Akawaambia, Ni maneno gani haya mnayosemezana hivi mnapotembea? Wakasimama wamekunja nyuso zao.

18Akajibu mmoja wao, jina lake Kleopa, akamwambia, Je! Wewe peke yako u mgeni katika Yerusalemu, hata huyajui yaliyotukia humo siku hizi?

19Akawauliza, Mambo gani? Wakamwambia, Mambo ya Yesu wa Nazareti, aliyekuwa mtu nabii, mwenye uwezo katika kutenda na kunena mbele za Mungu na watu wote;[#Mt 21:11]

20tena jinsi wakuu wa makuhani na wakubwa wetu walivyomtia katika hukumu ya kufa, wakamsulubisha.

21Nasi tulikuwa tukitumaini ya kuwa yeye ndiye atakayewakomboa Israeli. Zaidi ya hayo yote, leo ni siku ya tatu tangu yalipotendeka mambo hayo;[#Lk 1:68; 2:38; 19:11; Mdo 1:6]

22tena, wanawake kadhaa wa kwetu walitushitusha, waliokwenda kaburini asubuhi na mapema,[#Lk 24:1-11]

23wasiuone mwili wake; wakaja wakasema ya kwamba wametokewa na malaika waliosema kwamba yu hai.

24Na wengine waliokuwa pamoja nasi walikwenda kaburini wakaona vivyo hivyo kama wale wanawake walivyosema, ila yeye hawakumwona.[#Lk 24:12; Yn 20:3-10]

25Akawaambia, Enyi msiofahamu, wenye mioyo mizito ya kuamini yote waliyoyasema manabii!

26Je! Haikumpasa Kristo kupata mateso haya na kuingia katika utukufu wake?

27Akaanza kutoka Musa na manabii wote, akawaeleza katika maandiko yote mambo yaliyomhusu yeye mwenyewe.[#Kum 18:15; Zab 22:1-21; Isa 53:1-12]

28Wakakikaribia kile kijiji walichokuwa wakienda, naye alifanya kama anataka kuendelea mbele.

29Wakamshawishi wakisema, Kaa pamoja nasi, kwa kuwa kumekuchwa, na mchana unakwisha. Akaingia ndani kukaa nao.

30Ikawa alipokuwa ameketi nao chakulani, alitwaa mkate, akaubariki, akaumega, akawapa.[#Lk 22:19]

31Yakafumbuliwa macho yao, wakamtambua; kisha akatoweka mbele yao.

32Wakaambiana, Je! Mioyo yetu haikuwaka ndani yetu hapo alipokuwa akisema nasi njiani, na kutufunulia Maandiko?

33Wakaondoka saa ile ile, wakarejea Yerusalemu, wakawakuta wale kumi na mmoja wamekutanika, wao na wale waliokuwa pamoja nao,

34wakisema, Bwana amefufuka kweli kweli, naye amemtokea Simoni.[#1 Kor 15:4,5]

35Nao waliwapa habari ya mambo yale ya njiani, na jinsi alivyotambulikana nao katika kuumega mkate.

Yesu awatokea wanafunzi wake

36Na walipokuwa katika kusema habari hiyo, yeye mwenyewe alisimama katikati yao, akawaambia, Amani iwe kwenu.[#Mk 16:14-18; Yn 20:19-23; 1 Kor 15:5]

37Wakashituka, wakaogopa sana, wakidhani ya kwamba wanaona roho.[#Mt 14:26]

38Akawaambia, Mbona mnafadhaika? Na kwa nini mnaona shaka mioyoni mwenu?

39Tazameni mikono yangu na miguu yangu, ya kuwa ni mimi mwenyewe. Nishikenishikeni, mwone; kwa kuwa roho haina mwili na mifupa kama mnavyoniona mimi kuwa nayo.

40Na baada ya kusema hayo aliwaonesha mikono yake na miguu yake.

41Basi walipokuwa hawajaamini kwa furaha, huku wakistaajabu, aliwaambia, Mna chakula chochote hapa?

42Wakampa kipande cha samaki wa kuokwa.[#Yn 21:5,10]

43Akakitwaa, akala mbele yao.

44Kisha akawaambia, Hayo ndiyo maneno yangu niliyowaambia nilipokuwa ningali pamoja nanyi, ya kwamba ni lazima yatimizwe yote niliyoandikiwa katika Torati ya Musa, na katika vitabu vya Manabii na Zaburi.[#Lk 9:22,45; 18:31-33]

45Ndipo akawafunua akili zao wapate kuelewa maandiko.

46Akawaambia, Ndivyo ilivyoandikwa, kwamba Kristo atateswa na kufufuka siku ya tatu;[#1 Tim 3:16]

47na kwamba mataifa yote watahubiriwa kwa jina lake habari ya toba na ondoleo la dhambi, kuanza tangu Yerusalemu.

48Nanyi ndinyi mashahidi wa mambo haya.

49Na tazama, nawaletea juu yenu ahadi ya Baba yangu; lakini kaeni humu mjini, hadi mvikwe uwezo utokao juu.[#Mdo 1:4; Yn 15:26; 16:7]

Kupaa kwa Yesu

50Akawaongoza mpaka Bethania, akainua mikono yake akawabariki.[#Mdo 1:9-11]

51Ikawa katika kuwabariki, alijitenga nao; akachukuliwa juu mbinguni.

52Wakamwabudu; kisha wakarudi Yerusalemu wakiwa na furaha kuu.[#Yn 16:22; 14:28]

53Nao daima walikuwa ndani ya hekalu, wakimsifu Mungu.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya