The chat will start when you send the first message.
1Akaanza kusema nao kwa mifano; Mtu mmoja alipanda shamba la mizabibu, akalizungushia ua, akachimba shimo la shinikizo, akajenga mnara, akapangisha wakulima, akasafiri.[#Mt 21:33-46; Lk 20:9-19; #Isa 5:1-2]
2Na kwa wakati wake akatuma mtumwa kwa wale wakulima, ili apokee kwa wakulima katika matunda ya mizabibu.
3Wakamtwaa, wakampiga, wakamtoa nje, bila chochote.
4Akatuma tena kwao mtumwa mwingine, na huyo wakamtia majeraha ya kichwa, wakamfanyia jeuri.
5Akamtuma mwingine, huyo wakamwua; na wengine wengi, hawa wakiwapiga na hawa wakiwaua.
6Basi alikuwa na mmoja bado, mwana mpendwa wake; huyu naye akamtuma kwao mwisho, akisema, Watamstahi mwanangu.
7Lakini wale wakulima wakasemezana, Huyu ni mrithi; haya, na tumwue, na urithi utakuwa wetu.
8Wakamkamata, wakamwua, wakamtupa nje ya shamba la mizabibu.[#Ebr 13:12]
9Basi atafanyaje yule bwana wa shamba la mizabibu? Atakuja na kuwaangamiza wale wakulima, na lile shamba la mizabibu atawapa wengine.
10Hata andiko hili hamjalisoma,[#Zab 118:22-23]
Jiwe walilolikataa waashi,
Hilo limekuwa jiwe kuu la pembeni.
11Neno hili limetoka kwa Bwana,
Nalo ni ajabu machoni petu?
12Nao wakataka kumkamata, wakaogopa mkutano; maana walitambua ya kwamba ule mfano amewanenea wao. Wakamwacha wakaenda zao.
13Wakatuma kwake baadhi ya Mafarisayo na Maherodi, ili wamnase kwa maneno.[#Mt 22:15-22; Lk 20:20-26; #Mk 3:6]
14Hata walipofika walimwambia, Mwalimu, twajua ya kuwa wewe u mtu wa kweli, wala hujali cheo cha mtu; kwa maana hutazami sura za watu; lakini katika kweli waifundisha njia ya Mungu. Je! Ni halali kumpa Kaisari kodi au siyo?
15Tumpe, tusimpe? Naye, akijua unafiki wao, akawaambia, Mbona mmenijaribu? Nileteeni dinari niione.
16Wakaileta. Akawaambia, Ni ya nani sanamu hii na anwani hii? Wakamwambia, Ni ya Kaisari.
17Yesu akajibu, akawaambia, Mpeni Kaisari yaliyo ya Kaisari, na yaliyo ya Mungu mpeni Mungu. Wakamstaajabia sana.[#Rum 13:7]
18Kisha Masadukayo, watu wasemao ya kwamba hakuna kiyama, wakamwendea, wakamwuliza na kusema,[#Mdo 23:8; Mt 22:23-33; Lk 20:27-38]
19Mwalimu, Musa alituandikia ya kwamba ndugu ya mtu akifa, akamwacha mkewe wala hana mtoto, ndugu yake amtwae yule mkewe akampatie ndugu yake mzao.[#Kum 25:5,6; Mwa 38:8]
20Basi kulikuwa na ndugu saba, wa kwanza akatwaa mke, akafa, asiache mzawa.
21Wa pili naye akamtwaa akafa, wala yeye hakuacha mzawa. Na wa tatu kadhalika;
22hata na wote saba, wasiache mzawa. Mwisho wa wote yule mwanamke akafa naye.
23Basi, katika kiyama atakuwa mke wa yupi katika hao? Maana wote saba walikuwa naye.
24Yesu akajibu, akawaambia, Je! Hampotei kwa sababu hii, kwa kuwa hamyajui maandiko wala uweza wa Mungu?
25Kwa maana watakapofufuka katika wafu, hawaoi wala hawaolewi, bali huwa kama malaika walioko mbinguni.
26Na kuhusu wafu ya kwamba wafufuliwa, hamjasoma katika kitabu cha Musa, Kuhusu kile kichaka jinsi Mungu alivyomwambia, akisema, Mimi ni Mungu wa Abrahamu, na Mungu wa Isaka, na Mungu wa Yakobo?[#Kut 3:2,6; Mt 8:11; Lk 16:22]
27Yeye si Mungu wa wafu, bali wa walio hai. Hivyo mwapotea sana.
28Na mmojawapo wa waandishi akafika, akawasikia wakisemezana naye, akatambua ya kuwa amewajibu vema, akamwuliza, Katika amri zote ni ipi iliyo ya kwanza?[#Lk 10:25-28; Mt 22:34-40; Lk 20:39,40; #Lk 10:25-28]
29Yesu akamjibu, Ya kwanza ndiyo hii, Sikia, Israeli, Bwana Mungu wetu ni Bwana mmoja;[#Kum 6:4-5]
30nawe mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa akili zako zote, na kwa nguvu zako zote.[#Yn 15:12]
31Na ya pili ndiyo hii, Mpende jirani yako kama nafsi yako. Hakuna amri nyingine iliyo kuu kuliko hizi.[#Law 19:18]
32Yule mwandishi akamwambia, Hakika, Mwalimu, umesema vema ya kwamba Mungu ni mmoja, wala hakuna mwingine ila yeye;[#Kum 4:35; 6:4]
33na kumpenda yeye kwa moyo wote, na kwa ufahamu wote, na kwa nguvu zote, na kumpenda jirani kama nafsi yako, kwafaa kuliko sadaka nzima za kuteketezwa na dhabihu zote pia.[#Hos 6:6; 1 Sam 15:22]
34Naye Yesu, alipoona kwamba amejibu kwa busara, alimwambia, Wewe hu mbali na ufalme wa Mungu. Wala hakuthubutu mtu kumwuliza swali tena tokea hapo.[#Mdo 26:27-29]
35Yesu alipokuwa akifundisha katika hekalu, alijibu, akasema, Husemaje waandishi ya kwamba Kristo ni Mwana wa Daudi?[#Mt 22:41-46; Lk 20:41-44]
36Daudi mwenyewe alisema, kwa uweza wa Roho Mtakatifu,[#Zab 110:1; 2 Sam 23:2; Yn 7:42]
Bwana alimwambia Bwana wangu,
Uketi mkono wangu wa kulia,
Hata niwawekapo adui zako
Kuwa chini ya miguu yako.
37Daudi mwenyewe asema ni Bwana; basi amekuwaje mwanawe? Na watu wengi walikuwa wakimsikiliza kwa furaha.
38Akawaambia katika mafundisho yake, Jihadharini na waandishi, wapendao kutembea wakiwa wamevaa mavazi marefu, na kusalimiwa masokoni,[#Mt 23:1-39; Lk 20:45-47]
39na kuketi mbele katika masinagogi, na viti vya mbele katika karamu;
40ambao hula nyumba za wajane, na kwa unafiki husali sala ndefu; hawa watapata hukumu iliyo kubwa.
41Naye akaketi kulielekea sanduku la hazina, akatazama jinsi mkutano watiavyo mapesa katika sanduku. Matajiri wengi wakatia mengi.[#Lk 21:1-4; #2 Fal 12:9]
42Akaja mwanamke mmoja, mjane, maskini, akatia senti mbili, kiasi cha nusu pesa.
43Akawaita wanafunzi wake, akawaambia, Amin, nawaambia, Huyu mjane maskini ametia zaidi kuliko wote wanaotia katika sanduku la hazina;
44maana hao wote walitia baadhi ya mali iliyowazidi; bali huyu katika umaskini wake ametia vyote alivyokuwa navyo, ndiyo riziki yake yote pia.[#2 Kor 8:12]