Nehemia 2

Nehemia 2

Nehemia aenda Yuda

1Ikawa katika mwezi wa Nisani, mwaka wa ishirini wa mfalme Artashasta, na divai imewekwa mbele yake, nikaishika ile divai, nikampa mfalme. Nami mpaka sasa sikuwa na huzuni mbele ya mfalme wakati wowote.[#Ezr 7:1; #2:1 Mwezi wa kwanza katika kalenda ya Kiyahudi.]

2Basi mfalme akaniambia, Mbona umesikitika uso wako, nawe huna ugonjwa? Nini hii, isipokuwa ni huzuni ya moyo? Ndipo nikaogopa sana.[#Mit 15:13]

3Nikamwambia mfalme, Mfalme na aishi milele; kwani uso wangu usiwe na huzuni, iwapo mji, ulio mahali pa makaburi ya baba zangu, unakaa ukiwa, na malango yake yameteketezwa kwa moto?[#1 Fal 1:31; Dan 2:4; 5:10; Neh 1:3; Zab 137:5]

4Ndipo mfalme akaniambia, Una haja gani unayotaka kuniomba? Basi nikamwomba Mungu wa mbinguni.[#1 Sam 1:13; Mit 3:6]

5Nikamwambia mfalme, Mfalme akiona vema, na ikiwa mimi, mtumishi wako, nimepata kibali machoni pako, tafadhali unitume mpaka Yuda, niende katika mji wa makaburi ya baba zangu, nipate kuujenga.

6Mfalme akaniuliza, (malkia akiwa ameketi karibu naye), Safari yako itakuwa ya siku ngapi? Nawe utarudi lini? Hivyo mfalme akaona vema kunituma; nami nikampa muda.[#Neh 5:14]

7Tena nikamwambia mfalme, Mfalme akiona vema, na nipewe nyaraka kwa watawala walio ng'ambo ya Mto, ili wanikubalie kupita hadi nifike Yuda;

8nipewe na waraka kwa Asafu, mwenye kuutunza msitu wa mfalme, ili anipe miti ya kutengenezea boriti kwa malango ya ngome ya hekalu, na kwa ukuta wa mji; na kwa nyumba ile nitakapoishi mimi. Naye mfalme akanipa, maana mkono mwema wa Mungu wangu ulikuwa juu yangu.[#Ezr 10:6,9; Neh 3:7; Ezr 5:5; Mit 21:1; Isa 66:14; Dan 1:9; Mdo 7:10]

9Ndipo nikafika kwa watawala wa mkoa walio ng'ambo ya Mto, nikawapa nyaraka hizo za mfalme. Naye mfalme alikuwa ametuma maofisa wa jeshi lake na wapanda farasi pamoja nami.

10Hata Sanbalati, Mhoroni, na Tobia, mtumishi wake, Mwamoni, waliposikia habari hizi, ziliwahuzunisha sana, kwa kuwa amekuja mtu kuwatakia heri wana wa Israeli.

Nehemia akagua kuta za Yerusalemu

11Basi nikafika Yerusalemu, nikakaa huko muda wa siku tatu.[#Ezr 8:32]

12Kisha nikaondoka usiku, mimi pamoja na watu wachache; wala sikumwambia mtu neno hili alilolitia Mungu wangu moyoni mwangu, nilitende kwa ajili ya Yerusalemu; wala hapakuwa na mnyama pamoja nami, ila mnyama yule niliyempanda mwenyewe.

13Nikatoka nje usiku, kwa njia ya lango la bondeni, nikashika njia iendayo kwenye kisima cha joka, na lango la jaa; nikazitazama kuta za Yerusalemu, zilizokuwa zimebomoka; na malango yake yameteketezwa kwa moto.[#2 Nya 26:9; Neh 3:13; 1:3; Yer 5:10]

14Kisha nikaendelea mpaka lango la chemchemi, na ziwa la mfalme; lakini hapakuwa na nafasi ya kupita kwa yule mnyama niliyemganda.[#2 Fal 20:20; 2 Nya 32:30; Neh 3:15]

15Kisha nikapanda usiku kando ya kijito, nikautazama ukuta; kisha nikarudi nyuma, nikaingia kwa lango la bondeni, nikarejea hivyo.[#2 Sam 15:23; Yer 31:40; Yn 18:1]

16Wala maofisa hawakujua nilikokwenda, wala niliyotenda; tena nilikuwa sijawaambia Wayahudi, makuhani, wakuu, maofisa, wala watu wengine waliokuwa wakiifanya kazi hiyo.

Uamuzi wa kuzijenga kuta

17Kisha nikawaambia, Mnaona hali hii dhaifu tuliyo nayo, jinsi Yerusalemu ulivyo hali ya ukiwa, na malango yake yalivyoteketezwa kwa moto; haya! Na tuujenge tena ukuta wa Yerusalemu, ili tusiwe shutumu tena.[#1 Sam 11:2; Neh 1:3; Zab 44:13; Yer 24:9; Omb 3:45,46; Eze 5:14]

18Nikawaeleza habari ya mkono wa Mungu wangu ulivyokuwa mwema juu yangu; pia na maneno ya mfalme aliyoniambia. Nao wakasema, Haya! Na tuondoke tukajenge. Basi wakaitia mikono yao nguvu kwa kazi hiyo njema.[#2 Sam 2:7]

19Lakini Sanbalati, Mhoroni, na Tobia, mtumishi wake, Mwamoni, na Geshemu, Mwarabu, walitucheka, wakatudharau, wakasema, Ni nini neno hili mnalofanya? Je! Ninyi mtaasi juu ya mfalme?[#Zab 44:13; 79:4]

20Ndipo nikawajibu, nikawaambia, Mungu wa mbinguni, yeye atatufanikisha; kwa hiyo sisi, watumishi wake, tutaondoka na kujenga; lakini ninyi hamna sehemu, wala haki, wala kumbukumbu, katika Yerusalemu.[#Zab 127:1; Rum 8:31; Ezr 4:3; Yn 4:9; Mdo 8:21]

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya