Nehemia 5

Nehemia 5

Nehemia akabiliana na udhalimu

1Ndipo kukatokea kilio kikuu cha watu, na wake zao, juu ya ndugu zao Wayahudi.[#Isa 5:7; Yak 5:4; Law 25:35; Kum 15:7]

2Maana, walikuwako watu waliosema, Sisi, na wana wetu na binti zetu, tu wengi; na tupate ngano, tule, tukaishi.[#Mwa 41:57; Hag 1:6]

3Tena walikuwako wengine waliosema, Tumeweka rehani mashamba yetu, na mizabibu yetu, na nyumba zetu; tupate ngano, kwa sababu ya njaa.

4Tena walikuwako wengine waliosema, Tumekopa fedha ili kulipa kodi ya mfalme kwa kuweka rehani mashamba yetu, na mizabibu yetu.

5Walakini miili yetu ni kama miili ya ndugu zetu, na watoto wetu kama watoto wao; kumbe! Mnawatia utumwani wana wetu na binti zetu kuwa watumishi, na baadhi ya binti zetu wamekwisha kutiwa utumwani; wala hatuwezi kujiepusha na hayo; maana watu wengine wana mashamba yetu na mizabibu yetu.[#Mwa 37:27; Isa 58:7; Mdo 17:26; Kut 21:7; Mt 18:25]

6Nami nilikasirika sana, niliposikia kilio chao, na maneno hayo.[#Kut 11:8; Neh 13:8; Mk 3:5; Efe 4:26]

7Ndipo nikafanya shauri na nafsi yangu, nikagombana na wakuu na maofisa, nikawaambia, Nyote mnatoza watu riba, mtu na ndugu yake. Nikakutanisha mkutano mkubwa ili kukabiliana nao.[#Law 19:17; 1 Tim 5:20; Kut 22:25; Kum 23:19; Zab 15:5; Mit 27:5; Mt 18:17]

8Nikawaambia, Sisi kwa kadiri ya uwezo wetu tumewakomboa ndugu zetu Wayahudi, waliouzwa kwa makafiri; na ninyi mnataka kuwauza ndugu zenu, tena kuwauza ili sisi tuwanunue? Wakanyamaza kimya, wasiweze kusema neno lolote.[#Law 25:48]

9Tena nilisema, Neno hili mnalolitenda si jema; je! Haiwapasi ninyi kwenda katika kicho cha Mungu wetu, kwa sababu ya mashutumu ya makafiri adui zetu?[#Mwa 20:11; Law 25:36; Mdo 9:31; Mwa 13:7,8; 2 Sam 12:14; Rum 2:24; Tit 2:5; 1 Pet 2:12]

10Isitoshe mimi, ndugu zangu na watumishi wangu, tunawakopesha fedha na ngano ili kujipatia faida? Tafadhali na tuliache jambo hili la riba.

11Naomba, warudishieni hivi leo mashamba yao, mashamba yao ya mizabibu, mashamba yao ya mizeituni, nyumba zao, lile fungu la mia la fedha, la ngano, la divai, na la mafuta, mnalowatoza.

12Ndipo wakasema, Tutawarudishia, wala hatutataka kitu kwao; tutafanya hivyo, kama ulivyosema. Kisha nikawaita makuhani, nikawaapisha, ya kwamba watafanya kama walivyoahidi.[#Ezr 10:5; Yer 34:8,9]

13Tena nikakung'uta nguo yangu, nikasema, Mungu na amkung'ute vivyo hivyo kila mtu nyumbani mwake, na kazini mwake, asiyeitimiza ahadi hiyo; naam, na akung'utwe vivyo hivyo, na kuwa hana kitu. Mkutano wote wakasema, Amina; wakamhimidi BWANA. Nao watu wakafanya kama walivyoahidi.[#Mt 10:14; Mdo 13:51; Zek 5:4; 2 Fal 23:3]

Ukarimu wa Nehemia

14Tena tangu wakati huo nilipowekwa kuwa mtawala wao katika nchi ya Yuda, tangu mwaka wa ishirini hadi mwaka wa thelathini na mbili wa Artashasta mfalme, yaani, miaka kumi na miwili, mimi na ndugu zangu hatukula chakula cha mtawala.[#Neh 13:6; 1 Kor 9:4]

15Lakini watawala wa kwanza walionitangulia, wakawalemea watu, wakawatwalia chakula na mvinyo, zaidi ya shekeli arubaini za fedha; tena hata watumishi wao nao wakawatawala watu; lakini mimi sikufanya hivyo, kwa kuwa nilimcha Mungu.[#2 Kor 11:9; Mwa 42:18; Ayu 31:23; Zab 112:1; Mit 16:6; Mhu 12:13,14; Lk 18:2-4]

16Naam, hata kazi ya ukuta huu tena nikaishika sana, wala hatukujipatia mashamba; na watumishi wangu wote wakakusanyika huko kazini.

17Pamoja na hayo wakawako mezani pangu, katika Wayahudi na maofisa, watu mia moja na hamsini, zaidi ya wale waliotujia kutoka kwa mataifa yaliotuzunguka.[#2 Sam 9:7]

18Basi, maandalizi ya chakula yaliyoandaliwa kila siku yalikuwa ng'ombe mmoja na kondoo sita wazuri; tena nikaandaliwa kuku, na mara moja katika siku kumi akiba ya mvinyo ya namna zote; wala kwa hayo yote sikudai marupurupu ya chakula cha mtawala, kwa kuwa watu walikuwa wamebeba mzito mzito.[#1 Fal 4:22]

19Unikumbuke, Ee Mungu wangu, kwa mema, wote niliowatendea watu hawa.[#Neh 13:22]

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya