The chat will start when you send the first message.
1Kila mwanamke aliye na hekima hujenga nyumba yake;[#Rut 4:11; Mit 24:3,4]
Bali aliye mpumbavu huibomoa kwa mikono yake mwenyewe.
2Yeye aendaye kwa unyofu wake humcha BWANA;[#Ayu 12:4]
Bali aliye mkaidi katika njia zake humdharau.
3Katika kinywa cha mpumbavu mna fimbo ya kiburi,[#Mit 12:6]
Bali midomo ya wenye hekima huwahifadhi.
4Zizi ni safi ambapo hapana ng'ombe;
Bali nguvu za ng'ombe zaleta faida nyingi.
5Shahidi mwaminifu hatasema uongo;[#Kut 20:16]
Bali shahidi wa uongo, pumzi zake ni uongo.
6Mwenye dharau hutafuta hekima, asiipate;[#Mit 17:24]
Bali maarifa huwa mepesi kwa mwenye ufahamu.
7Toka mbele ya uso wa mpumbavu,
Maana hutaona kwake midomo ya maarifa.
8Akili za mwenye busara ni kujua njia yake;[#Lk 12:20; 1 Kor 3:19]
Lakini upumbavu wa wapumbavu ni udanganyifu.
9Wapumbavu huidharau hatia;[#Mit 1:22]
Bali upo upendeleo kwa wenye haki.
10Moyo huujua uchungu wa nafsi yake,
Wala mgeni haishiriki furaha yake.
11Nyumba ya mtu mwovu itabomolewa;[#Ayu 8:15; Mit 3:33]
Bali hema la mwenye haki litafanikiwa.
12Iko njia ionekanayo kuwa sawa machoni pa mtu,[#Mit 16:25; Rum 6:21]
Lakini mwisho wake ni njia za mauti.
13Hata wakati wa kucheka moyo huwa na huzuni;[#Mhu 2:2]
Na mwisho wa furaha ni uzito wa moyo.
14Ageukaye moyoni hushiba njia zake mwenyewe;[#Mit 12:14; 2 Kor 1:12; Flp 4:7]
Na mtu mwema ataridhika nafsini mwake.
15Mjinga huamini kila neno;
Bali mwenye busara huangalia sana aendavyo.
16Mwenye hekima huhadhari, na kujitenga na uovu;[#Mit 22:3]
Bali mpumbavu hupuuza yote, na hajali.
17Yeye aonaye hasira upesi atatenda kwa ujinga;
Na mtu mwenye hila mbaya huzirwa.
18Wajinga hurithi upumbavu;
Bali wenye busara huvikwa taji la maarifa.
19Wabaya huinama mbele ya wema,
Na wasio haki malangoni mwao wenye haki.
20Maskini huchukiwa hata na jirani yake;[#Mit 19:7]
Bali tajiri ana marafiki wengi.
21Amdharauye mwenzake afanya dhambi;[#Zab 41:1]
Bali amhurumiaye maskini ana heri.
22Je! Hawakosi wawazao mabaya?
Bali fadhili na kweli zina wao wawazao mema.
23Katika kila kazi mna faida;
Bali maneno ya midomo huleta hasara tu.
24Taji la wenye hekima ni mali zao;
Bali upumbavu wa wajinga ni upumbavu tu.
25Shahidi wa kweli huponya nafsi za watu;
Bali atoaye uongo hudanganya.
26Kumcha BWANA ni tumaini imara;
Watoto wake watakuwa na kimbilio.
27Kumcha BWANA ni chemchemi ya uzima,[#Mit 13:14]
Ili kuepukana na tanzi za mauti.
28Utukufu wa mfalme ni wingi wa watu wake;
Bali uchache wa watu ni uharibifu wa mkuu wao.
29Asiye mwepesi wa hasira ana fahamu nyingi;[#Mit 15:18; Mt 11:29; 1 Kor 13:4,5; Yak 1:19]
Bali mwenye roho ya hamaki hutukuza upumbavu.
30Moyo ulio mzima ni uhai wa mwili;[#Ayu 5:2; Zab 112:10; Mdo 7:9; Rum 1:29; Yak 4:5]
Bali husuda ni ubovu wa mifupa.
31Amwoneaye maskini humsuta Muumba wake;[#Ayu 31:15,16; Mhu 5:8; Mit 17:5; 22:2; Mt 25:40; 1 Yoh 3:17]
Bali yeye awahurumiaye wahitaji humheshimu.
32Mtu mbaya husukumwa chini katika kutenda mabaya kwake;[#Ayu 13:15; Zab 23:4; 2 Kor 1:9; 2 Tim 4:18]
Bali mwenye haki ana matumaini katika kufa kwake.
33Hekima hukaa katika moyo wake mwenye ufahamu;
Bali yaliyo ndani ya wapumbavu hudhihirika.
34Haki huinua taifa;
Bali dhambi ni aibu ya watu wowote.
35Upendeleo wa mfalme humwelekea mtumwa atendaye kwa busara;[#Mt 24:45-47]
Bali hasira yake itakuwa juu yake aletaye aibu.